Zenj FM
Zenj FM
20 November 2026, 13:11

Wananchi wa Manispaa ya Kati wametakiwa kupata vibali vya ujenzi kabla ya kuanza kujenga nyumba, maduka na majengo mengine ili kuepuka faini na migogoro ya ardhi. Hatua hiyo inalenga kuimarisha mipango ya mji, kuongeza mapato ya Manispaa na kuhakikisha ujenzi unazingatia taratibu zilizowekwa.
Na Mwandishi wetu
Wananchi wanaotaka kujenga nyumba, maduka, kuta na majengo mengine wametakiwa kufika katika ofisi za Manispaa ya Kati kabla ya kuanza ujenzi, ili kupata mwongozo wa wataalamu wa mipango miji, kujua maeneo yanayofaa kwa ujenzi, pamoja na taratibu za kupata vibali na kufanya malipo husika.
Wito huo umetolewa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kati, Said Hassan Shaaban, wakati wa kikao cha Kamati ya Fedha cha Manispaa hiyo, kilichojadili mwenendo wa mapato na matumizi kwa mwezi Oktoba 2026, pamoja na mwelekeo wa matumizi kwa mwezi Novemba.
Amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakianza ujenzi bila kuwa na vibali rasmi, hali inayokiuka taratibu zilizowekwa na inayoweza kusababisha faini pamoja na usumbufu kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa ya Kati, Mwanaisha Ali Said, amesema wajumbe wa kamati hiyo wamehimiza kuimarishwa kwa ukusanyaji wa mapato yatokanayo na vibali vya ujenzi, huku wananchi wakikumbushwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa.
Amesema kamati imeelekeza kuundwa kwa timu maalumu itakayofuatilia na kuhamasisha wananchi kupata vibali vya ujenzi, hatua inayolenga kuimarisha mpangilio wa mji na kupunguza migogoro ya ardhi.
Naye Mkuu wa Divisheni ya Mapato, Uchumi na Wajasiriamali wa Baraza la Manispaa ya Kati, Mussa Abdurabi Fadhili, amesema ukusanyaji wa mapato umevuka makadirio kutokana na ufuatiliaji uliofanyika katika maeneo mbalimbali pamoja na ushirikiano ulioimarishwa na masheha katika usimamizi na utoaji wa vyeti vya mazao.
Aidha, amewahimiza wananchi kuhakikisha wanapata vibali vya ujenzi kabla ya kuanza kazi za ujenzi, hususan katika kipindi hiki cha masika.