Zenj FM

Enabel yawakabidhi vifaa vya tehama wasaidizi wa sheria Unguja, Pemba

12 August 2026, 20:59

Kaimu Katibu wa Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Omar Haji Gora akiwa na wajumbe wa bodi wa ZAPONET pamoja na kiongozi wa ENABEL

Wasaidizi wa sheria katika wilaya 11 za Unguja na Pemba wamekabidhiwa vifaa vya TEHAMA kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kazi na kuboresha huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi.
Vifaa hivyo vinajumuisha laptop 33, desktop 33, tablet 22, mashine moja ya fotokopi na router 11, vilivyotolewa kupitia mradi wa Sauti ya Mwanamke.Wadau wameeleza kuwa vifaa hivyo vitasaidia kuwafikia zaidi wanawake na watoto wanaohitaji huduma za msaada wa kisheria.

Na Mary Julius.

Wasaidizi wa sheria katika wilaya 11 za Unguja na Pemba wamekabidhiwa vifaa vya TEHAMA vyenye thamani ya kuongeza ufanisi wa kazi na kurahisisha utoaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi, hususan wanawake na watoto.

Vifaa hivyo, vilivyotolewa kupitia mradi wa Sauti ya Mwanamke, unaotekelezwa na  Enabel, EU, ZAPONET na Serikali, vinajumuisha laptop 33, desktop 33, tablet 22, mashine moja ya fotokopi na router 11.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika ukumbi wa wizara, Kaimu Katibu wa Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Omar Haji Gora, amesema matumizi ya teknolojia ni muhimu katika kuendana na kasi ya maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi.

Amesema mabadiliko ya kiteknolojia yanahitaji taasisi na watendaji kutumia mifumo ya kisasa ili kuongeza ufanisi, huku akieleza kuwa vifaa hivyo vitasaidia katika utendaji wa kazi, ukusanyaji na uhifadhi wa takwimu sahihi pamoja na utoaji wa huduma bora za msaada wa kisheria.

Omar amewataka wasaidizi wa sheria kuvitumia na kuvitunza vifaa hivyo kwa malengo yaliyokusudiwa, akisisitiza kuwa mahitaji ya huduma za msaada wa kisheria yanaendelea kuongezeka.

Sauti ya Kaimu Katibu wa Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Omar Haji Gora.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Enabel, Virginie Hallet, amesema mradi wa Sauti ya Mwanamke ni uwekezaji unaolenga kuwajengea uwezo wasaidizi wa sheria ili waweze kuwafikia wanawake na kuwapatia huduma za msaada wa kisheria kwa ufanisi zaidi.

Amesema vifaa hivyo vimesambazwa katika wilaya za Unguja na Pemba kwa lengo la kuwawezesha wasaidizi wa sheria kufanya kazi zao kwa ufanisi na kuwafikia wananchi wenye uhitaji wa huduma hizo.

Mwakilishi Mkazi wa Enabel, Virginie Hallet

Naye Jesca Msafiri kutoka UN Women amesema UN Women, ZAPONET na Enabel wameendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha juhudi za kulinda na kupigania haki za wanawake na watoto.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mvuli wa Wasaidizi wa Kisheria, Asia Abdulsalam Hussein, amesema msaada huo kutoka Enabel kupitia mradi wa Sauti ya Mwanamke, ambao sehemu yake inafadhiliwa na Umoja wa Mataifa, ni sehemu ya juhudi za kuijengea uwezo ZAPONET na wasaidizi wa sheria.

Asia amesema vifaa hivyo vitawawezesha wasaidizi wa sheria kutoa huduma kwa usahihi, kwa wakati na kwa kuzingatia weledi.

Ameishukuru Enabel kwa msaada huo, akisema ushirikiano huo hauishii katika utoaji wa vifaa pekee, bali unaenda sambamba na juhudi za muda mrefu za kuboresha huduma za msaada wa kisheria.

Aidha, amewataka wasaidizi wa sheria kuvitunza vifaa hivyo na kuhakikisha vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, huku akisema ZAPONET itaendelea kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika kuboresha utendaji wa kazi na huduma za kidijitali.

Asia pia ameiomba Enabel pamoja na wadau wengine kuendelea kushirikiana na ZAPONET, akieleza kuwa bado kuna mahitaji makubwa yanayohitaji nguvu za pamoja.

Akitoa neno la shukrani, Othuman Abassi ameishukuru Serikali na wadau kwa kuwezesha upatikanaji wa vifaa hivyo, huku akiomba Serikali kusaidia kutafuta namna ya kuwapatia wasaidizi wa sheria ofisi katika kila wilaya, ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Ameahidi kuwa vifaa hivyo vitatunzwa na kutumika kwa mujibu wa malengo yaliyokusudiwa, kwa manufaa ya wananchi wanaohitaji huduma za msaada wa kisheria.

Sauti ya Othuman Abassi.