Zenj FM
Zenj FM
30 July 2026, 23:00

Baada ya taarifa za mtoto Jamal kusambaa mitandaoni akiomba msaada wa matibabu, Mbunge wa Jimbo la Fuoni, Asha Hussein Saleh, amejitokeza kumtembelea na kumpeleka Hospitali ya Lumumba kwa uchunguzi na matibabu. Madaktari wamebaini kuwa uvimbe alionao si saratani na mtoto huyo anaendelea kupatiwa huduma za matibabu.
Na Mary Julius.
Baada ya kusambaa kwa taarifa katika mitandao ya kijamii kuhusu mtoto Jamal, mkazi wa Fuoni Chunga, aliyekuwa akiomba msaada wa matibabu kutokana na uvimbe kwenye jicho lake la kushoto, Mbunge wa Jimbo la Fuoni, Asha Hussein Saleh, amechukua hatua ya kumtembelea nyumbani na baadaye kumpeleka Hospitali ya Lumumba kwa ajili ya matibabu.
Mbunge Asha amesema alipata taarifa za hali ya mtoto huyo kupitia mitandao ya kijamii, jambo lililomsukuma kufika nyumbani kwa Jamal ili kujionea hali yake.
Baada ya kushuhudia changamoto aliyokuwa nayo, aliamua kumpeleka Hospitali ya Lumumba ambako madaktari wamempokea, wakamfanyia uchunguzi na kumlaza kwa ajili ya kuendelea na matibabu.
Mbunge Asha Saleh amewasihi wananchi wa Zanzibar kuwahi kufika katika vituo vya afya wanapopata changamoto za kiafya, akieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, imeendelea kuimarisha huduma za afya ili wananchi wapate matibabu bora na kwa wakati.
Aidha, amesema pale changamoto zinaposhindikana kutatuliwa katika ngazi za kawaida, wananchi wanapaswa kuwafikia viongozi wa majimbo yao kwa kuwa wako tayari kushirikiana nao na kuwasaidia kupata suluhisho la matatizo yanayowakabili.
Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Macho katika Hospitali ya Lumumba, Dkt. Yusuf Said Ahmed, amesema baada ya kumpokea Jamal na kufanya uchunguzi wa awali, wamebaini kuwa uvimbe alionao unahusisha neva za jicho na si ugonjwa wa saratani.
Naye Amier Suleiman Khamis, ambaye aliibua changamoto ya Jamal kupitia mitandao ya kijamii, amesema anashukuru kwa hatua ya haraka iliyochukuliwa na Mbunge wa Jimbo la Fuoni, akieleza kuwa msaada huo umeleta matumaini mapya kwa mtoto huyo na familia yake kupata matibabu yanayohitajika.