Zenj FM
Zenj FM
20 May 2026, 16:19

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Hamza Hassan Juma amesema Serikali kupitia Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) itaendelea kuhamasisha matumizi ya vipimo sahihi ili kujenga mazingira ya biashara yenye haki na usawa. Aidha, amewataka wafanyabiashara kushirikiana na wakala huo kwa kuhakikisha vipimo vyao vinakaguliwa mara kwa mara ili kuondoa udanganyifu.
Na Mary Julius.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Sera na Uratibu wa Baraza la Wawakilishi Hamza Hassan Juma amesema mafanikio ya biashara pamoja na ukuaji wa uchumi wa Zanzibar yanategemea matumizi sahihi ya vipimo, huku akisisitiza kuwa jukumu hilo linahitaji ushirikiano wa Serikali kupitia Wakala wa Vipimo Zanzibar, ZAWEMA wafanyabiashara pamoja na wananchi kwa ujumla.
Amesema hayo katika Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani lililofanyika katika Ukumbi wa ZSSF Kariakoo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku hiyo yanayofanyika kila mwaka tarehe 20 Mei.
Waziri Hamza amesema Serikali itaendelea kuhamasisha matumizi sahihi ya vipimo pamoja na kuwasaidia wafanyabiashara, waagiziaji, wazalishaji wa bidhaa na wajasiriamali kuhakikisha bidhaa wanazoziagiza au kuzizalisha zinazingatia matakwa ya vipimo sahihi katika ufungashaji wake ili kujenga mazingira ya biashara yenye haki na usawa.
Aidha, ametoa wito kwa wafanyabiashara wanaotumia vipimo kuendelea kushirikiana na Wakala wa Vipimo kwa kuhakikisha vipimo wanavyovitumia vinawasilishwa katika vipindi vya ukaguzi pamoja na kujenga utamaduni wa kujiridhisha mara kwa mara kama bado vinafanya kazi kwa usahihi kabla ya wakaguzi kufika katika maeneo yao ya biashara.
Akizungumzia kauli mbiu ya mwaka huu isemayo “Sayansi ya Vipimo: Hujenga Uaminifu katika Uandaaji wa Sera”, Waziri Hamza amesema kauli hiyo inaonesha wazi kuwa masuala ya vipimo ni sekta mtambuka inayogusa shughuli zote za kila siku pamoja na utekelezaji wa sera mbalimbali za maendeleo.
Amesema utekelezaji na mafanikio ya sera hupimwa kwa matokeo yake, hivyo matumizi ya vipimo sahihi yana mchango mkubwa katika kutoa tathmini sahihi ya utekelezaji wa sera hizo na kujenga uaminifu katika maamuzi yanayofanywa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Zanzibar ZAWEMA Mohammed Simai amesema matumizi ya vipimo yana historia kubwa duniani na kwamba sekta hiyo ni miongoni mwa sekta mtambuka zinazogusa maisha ya kila siku ya wananchi.
Amesema katika Wiki ya Vipimo, ZAWEMA kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar wamefanya uhakiki wa vipimo katika sekta ya afya ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinazingatia usahihi wa vipimo.
Aidha mkurugenzi ameelezea baadhi ya ya malalamiko ya baadhi ya wafanya biashara hasa wa mchanga wa ujenzi dhidi ya kipimo kinacho tumiwa na moja ya idara ya wizara maji nishati na madini ambacho hakiendani usahihi wa matumizi yake kwa huduma wanazo zitoa.
Katika kongamano hilo, Amour Yussuf Ramadhan akiwasilisha mada kuhusu “Vipimo katika Uislamu”, amesema dini ya Kiislamu imeweka msisitizo mkubwa katika matumizi sahihi ya vipimo na mizani huku akionya madhara ya udanganyifu katika vipimo.
Naye Gérard Mushi kutoka Wakala wa Vipimo Tanzania Bara amesema vipimo vinatumika katika maisha ya kila siku ikiwemo biashara, afya, maji, umeme na usalama wa jamii, huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha vifaa vya tiba na vipimo vinahakikiwa kwa usahihi ili wananchi wapate huduma bora na salama.