Zenj FM

Jitimai yajivunia huduma bora za afya, wito watolewa kufuata mfumo wa rufaa

20 July 2026, 20:15

Daktari Dhamana wa Hospitali ya Wilaya ya Jitimai na Daktari Bingwa wa Upasuaji, Dk. Shabbir Adamjee,

Hospitali ya Wilaya ya Jitimai imewahimiza wananchi kuzingatia mfumo wa rufaa ili kuboresha utoaji wa huduma za afya na kupunguza msongamano wa wagonjwa. Uongozi wa hospitali umeeleza hospital hiyo inatoa huduma mbalimbali za kibingwa, dharura na kliniki maalumu, ikiwemo Kliniki ya Magonjwa ya Damu iliyoimarishwa kwa vifaa vya kisasa na dawa za kutosha.

Na Mary Julius.

Uongozi wa Hospitali ya Wilaya ya Jitimai umewataka wananchi kuzingatia mfumo wa rufaa wanapohitaji huduma za afya, ukieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa na kuboresha utoaji wa huduma hospitalini.

Akizungumza na waandishi wa habari, Msaidizi wa Dhamana wa Hospitali ya Wilaya ya Jitimai, Dk. Abdallah Khamis Machano, amesema hospitali Jitimai ni ya ngazi ya wilaya inayopokea wagonjwa waliopata rufaa kutoka zahanati na vituo vya afya, isipokuwa kwa wagonjwa wa dharura na wanaohitaji huduma za kibingwa ambao hupokelewa moja kwa moja.

Amesema hospitali hiyo inaendelea kutoa huduma mbalimbali za afya zikiwemo huduma za kibingwa, matibabu ya wagonjwa wa nje, huduma za dharura pamoja na huduma za wagonjwa waliolazwa.

Ameeleza kuwa hospitali hiyo pia hutoa huduma za lishe na chakula kwa wagonjwa waliolazwa na ndugu wanaowahudumia, huku ikitumika kama kituo cha mafunzo kwa wanafunzi wa kada mbalimbali za afya wanaofika kujifunza kwa vitendo.

Dk. Machano amesema Hospitali ya Wilaya ya Jitimai ina wataalamu katika idara mbalimbali zikiwemo watoto, upasuaji, afya ya mama na mtoto, huduma za wajawazito, lishe, magonjwa ya damu pamoja na madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali.

Sauti ya Msaidizi wa Dhamana wa Hospitali ya Wilaya ya Jitimai, Dk. Abdallah Khamis Machano,

Kwa upande wake, Daktari Dhamana wa Hospitali ya Wilaya ya Jitimai na Daktari Bingwa wa Upasuaji, Dk. Shabbir Adamjee, amesema hospitali hiyo ilianzishwa kwa maono ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa lengo la kusogeza huduma bora za afya karibu na wananchi.

Dk. Adamjee amesema hospitali hiyo imeendelea kuhudumia wananchi kutoka maeneo mbalimbali kwa kutoa huduma za dharura, magonjwa ya ndani, afya ya mama na mtoto, huduma za wajawazito, magonjwa ya mfumo wa chakula, ngozi, mifupa pamoja na huduma nyingine za kibingwa.

Sauti ya Daktari Dhamana wa Hospitali ya Wilaya ya Jitimai na Daktari Bingwa wa Upasuaji, Dk. Shabbir Adamjee,

Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi, Dk. Shahizma Abdulhakim Omar, amesema hospitali hiyo inaendelea kutoa huduma za kisasa za afya ya uzazi na wanawake, zikiwemo uchunguzi, matibabu na ushauri wa kitaalamu kwa wanawake wanaofika hospitalini, huku akiwahimiza wanawake kujitokeza mapema wanapopata changamoto za kiafya ili kupata matibabu stahiki.

Sauti ya Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi, Dk. Shahizma Abdulhakim Omar.

Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu, Dk. Mohammed Said Suleimani, amewataka wagonjwa waliokuwa wakihudhuria Kliniki ya Magonjwa ya Damu katika Hospitali ya Mnazi Mmoja kuendelea kupata huduma katika Kliniki ya Magonjwa ya Damu ya Hospitali ya Wilaya ya Jitimai.

Dk. Mohammed amesema kliniki hiyo imeboreshwa kwa kiwango kikubwa na sasa ina dawa za kutosha, maabara ya kisasa pamoja na sehemu maalumu ya kutolea dawa, hatua inayorahisisha upatikanaji wa huduma kwa wagonjwa.

Amehimiza wananchi wenye matatizo ya damu kufika hospitalini kwa ajili ya uchunguzi wa kina, ushauri wa kitaalamu na matibabu sahihi.

Aidha, amewashauri wanandoa wanaotarajia kufunga ndoa kupima vinasaba (genotype) kabla ya kuoana ili kupunguza hatari ya kurithisha magonjwa ya damu kwa watoto watakaozaliwa.

Sauti ya Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu, Dk. Mohammed Said Suleimani.

Nao baadhi ya wagonjwa wanaohudhuria kliniki hiyo, akiwemo Rehema na Mariamu Juma, wameelezea kuridhishwa na huduma wanazopatiwa hospitalini hapo.

Sauti wagonjwa.