Zenj FM
Zenj FM
4 May 2026, 5:08 pm

Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) kwa kushirikiana na UNCTAD na UN DESA imeendesha semina ya siku mbili kwa watendaji wake ili kuwajengea uwezo wa kutambua vyanzo vya fedha na kuandaa miradi yenye mvuto kwa wawekezaji, hususan katika sekta ya nishati jadidifu.
Na Mary Julius.
Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mkutano wa Biashara na Maendeleo (UNCTAD) pamoja na Idara ya Masuala ya Kiuchumi na Kijamii ya Umoja wa Mataifa (UN DESA), imeandaa semina ya siku mbili kwa watendaji wake, ikiwa na lengo la kuwajengea uwezo katika kutambua vyanzo vya fedha, namna ya kuvifikia, pamoja na kuandaa miradi yenye mvuto kwa wawekezaji, hususan katika sekta ya nishati jadidifu.
Akifungua semina hiyo kwa niaba ya Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Katibu Mkuu wa wizara hiyo Khamis Suleimani Mwalimu amesema Zanzibar ipo katika kipindi muhimu cha mageuzi ya kiuchumi chini ya uongozi wa Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ambapo inalenga kuwa kitovu cha uwekezaji endelevu, ukuaji wa viwanda na uchumi wa kijani.
Amesema Serikali imeweka mkazo mkubwa katika sekta ya nishati kama mhimili wa maendeleo, akibainisha kuwa bila nishati ya uhakika, nafuu na endelevu, juhudi za kukuza viwanda na kuvutia uwekezaji hazitaweza kufanikiwa kikamilifu.
Waziri amesema Nishati jadidifu, hususan nishati ya jua na upepo, imeelezwa kuwa kipaumbele cha kimkakati katika ajenda ya taifa, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha utekelezaji wa miradi na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Richard Muyungi, amesema Serikali inaendelea kushirikiana na taasisi za kimataifa katika kutafuta rasilimali fedha za maendeleo, hususan katika miradi ya nishati safi na mazingira.
Ameeleza kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuongeza uelewa kwa watendaji wa ZIPA, hasa vijana, katika kuandaa miradi yenye ubunifu na tija, itakayochangia kupunguza gesi chafuzi na kuimarisha uchumi wa kijani.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ZIPA, Saleh Saad Mohamed, amesema mafunzo hayo yanalenga kuongeza ufanisi katika kuvutia uwekezaji kwenye nishati mbadala, akibainisha kuwa katika miaka mitano iliyopita, ZIPA imesajili zaidi ya miradi 630 inayohitaji nishati ya uhakika.
Aidha Mkurugenzi Saleh amesema Mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza uwezo wa watendaji wa ZIPA katika kubuni na kusimamia miradi yenye tija, sambamba na kuimarisha nafasi ya Zanzibar katika sekta ya uwekezaji wa nishati safi na endelevu.

Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar ZECO Haji Haji amesema kuwa semina hiyo itasaidia kuongeza uelewa kuhusu namna sekta binafsi inavyoweza kushiriki kikamilifu katika uwekezaji wa uzalishaji wa umeme nchini.
Meneja amesema kwa sasa Zanzibar inapokea umeme kutoka tanesco takribani megawati 135.7,hata hivyo, amesema mahitaji halisi ya umeme ni megawati 165, hali inayosababisha upungufu wa takribani megawati 30.
Aidha amesisitiza kuwa hali hiyo inaonesha wazi umuhimu wa kutafuta njia mbadala za kuzalisha umeme wa kutosha na endelevu ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka sambamba na ukuaji wa uchumi.