Zenj FM

Wakazi Uroa gizani kufuatia wizi wa transfoma, serikali yachukua hatua

4 May 2026, 5:26 pm

Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar ZECO Haji Haji.

Meneja wa ZECO, Haji Haji, amewataka wananchi kuacha mara moja kuharibu miundombinu ya umeme visiwani Zanzibar akibainisha kuwa vitendo hivyo vinaleta hasara kubwa kwa Serikali.

Na Mary Julius.

Meneja wa Shirika la Umeme Zanzibar ZECO Haji Haji amewataka wananchi kuacha mara moja vitendo vya kuharibu miundombinu ya umeme iliyowekwa katika maeneo mbalimbali visiwani humo, akisema kuwa vitendo hivyo vinaisababishia Serikali hasara kubwa.

Mmeneja Haji ameyasema hayo pembezoni mwa semina ya wafanyakazi wa ZIPA iliyofanyika Madinat Al Bahr.

Ameeleza kuwa kumekuwa na ongezeko la matukio ya wizi na uharibifu wa transfoma, hususan katika eneo la Uroa.

Amefafanua kuwa wahalifu wanaohusika na wizi huo hulenga kuiba shaba iliyopo ndani ya transfoma, ambayo thamani yake haizidi shilingi laki mbili, huku wakisababisha uharibifu wa transfoma yenye thamani inayofikia shilingi milioni 23.

Aidha, ameongeza kuwa uharibifu wa transfoma hiyo umepelekea wakazi wa Uroa kukosa huduma ya umeme, jambo lililosababisha hasara kubwa kwa wananchi, hususan wafanyabiashara wanaotegemea umeme katika shughuli zao za kila siku.

Meneja mkuu haji amewasisitiza wananchi kushirikiana na vyombo vya dola kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na vitendo hivyo ili kulinda miundombinu ya umeme na kuhakikisha huduma inaendelea kutolewa kwa ufanisi.

Sauti ya Meneja ZECO Haji Haji.