Zenj FM
Zenj FM
24 April 2026, 9:49 pm

Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff, amesema Tamasha la Uwekezaji Zanzibar 2026 litakuwa jukwaa muhimu la kukuza uchumi na maendeleo endelevu. Tamasha hilo, lililoandaliwa na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar, litafanyika kuanzia Juni 3 hadi 5, 2026 katika Ukumbi wa Golden Tulip Zanzibar Airport.
Na Mary Julius.
Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff, amesema kuwa Tamasha la Uwekezaji Zanzibar 2026 linatarajiwa kuwa jukwaa muhimu litakalofungua ukurasa mpya wa ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu ya Zanzibar.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, katika ukumbi wa wizara hiyo Waziri shariff amesema kuwa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar imeandaa tamasha hilo litakalofanyika kuanzia tarehe 3 hadi 5 Juni 2026 katika Ukumbi wa Golden Tulip Zanzibar Airport.
Tamasha hilo linatarajiwa kukutanisha zaidi ya washiriki 500 kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwemo wawekezaji wa kimataifa, watunga sera, wafanyabiashara wakubwa, washirika wa maendeleo pamoja na wanadiaspora.
Kwa mujibu wa Waziri Shariff, tamasha hilo litakuwa jukwaa la kimataifa linalolenga kuhamasisha fursa za uwekezaji na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kwa maendeleo endelevu ya Zanzibar.
Tamasha hilo litafunguliwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi, ikiwa ni ishara ya dhamira thabiti ya Serikali katika kukuza uwekezaji unaoongozwa na sekta binafsi.
Tamasha hilo linaongozwa na kaulimbiu isemayo,“Promoting Investment Diversification for Sustainable Development in Zanzibar: Shaping Zanzibar’s Next Growth Story.”
Katika hatua nyingine waziri sharif amesema ZIPA imetangaza mashindano ya kubuni nembo ya Tamasha la Uwekezaji Zanzibar 2026.
Mshindi atajishindia shilingi milioni 2 za Kitanzania pamoja na kutambuliwa rasmi katika hafla ya Gala Dinner.