Zenj FM

Mambosasa walia na vitendo vya kihalifu.

17 June 2026, 15:28

Jengo la afisi ya sheha wa shehia ya Mambosasa.

Safia Mohamed.

Wananchi wa Shehia ya Fuoni Mambo Sasa wameilalamikia serikali kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya kihalifu vinavyoendelea kujitokeza katika eneo lao.

Wakizungumza na waandishi wa habari katika mahojiano yaliyofanyika katika ofisi ya Sheha wa Shehia ya Fuoni Mambo Sasa, Mkoa wa Magharibi B, Unguja, wananchi hao wamesema kuwa changamoto ya uporaji imekuwa ikidumu kwa muda mrefu, hali inayowanyima amani na kuhatarisha usalama wa maisha pamoja na mali zao.

Wananchi hao wameeleza kuwa sababu kubwa zinazochangia kuwepo kwa vitendo hivyo ni mmomonyoko wa maadili pamoja na ukosefu wa ajira kwa vijana, jambo linalowasukuma baadhi yao kujiingiza katika vitendo vya uhalifu.

Mwananchi.

Kwa upande wake, Sheha wa Shehia ya Fuoni Mambo Sasa, Asya Omar Mohd, amesema kuwa tayari hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa kukabiliana na tatizo hilo, ikiwemo kuunda kikosi cha ulinzi shirikishi cha shehia kwa lengo la kupunguza na kudhibiti vitendo vya kihalifu.

Sauti ya Sheha wa Shehia ya Fuoni Mambo Sasa, Asya Omar Mohd,

Naye Mwenyekiti wa Polisi Jamii wa Shehia ya Fuoni Mambo Sasa, Seif Suleiman Abdallah, amesema kuwa kikosi hicho kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kinaendelea kufanya doria za mara kwa mara katika shehia hiyo ili kuimarisha usalama na kupunguza matukio ya uhalifu.

Aidha, amebainisha kuwa ukosefu wa ushirikiano kutoka kwa baadhi ya wananchi kwa vyombo vya ulinzi na usalama unachangia kuwepo kwa changamoto katika utekelezaji wa majukumu yao.

Kutokana na hali hiyo, amewataka wananchi kuondoa tabia ya kuwaficha wahalifu na badala yake kutoa taarifa kwa vyombo husika ili kusaidia mapambano dhidi ya uhalifu.

SAuti ya Mwenyekiti wa Polisi Jamii wa Shehia ya Fuoni Mambo Sasa, Seif Suleiman Abdallah.