Zenj FM

Rais Mwinyi kuing’arisha mei mosi Zanzibar

28 April 2026, 1:04 pm

Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Sharriff A. Sharriff akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake. Mwanakwerekwe.

Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Mei Mosi yatakayofanyika Viwanja vya Dole.Maadhimisho hayo yatapambwa na maandamano pamoja na maonyesho kutoka taasisi za umma na binafsi.

Na Mary Julius.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yatakayofanyika katika Viwanja vya Dole, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Akizungumza ofisini kwake Mwanakwerekwe, Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Sharriff A. Sharriff amesema Serikali ya Awamu ya Nane chini ya uongozi wa Rais Dkt. Mwinyi inaendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi, ikitambua mchango wao kama nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa.

Waziri Sharriff amewakaribisha wananchi wote kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo yatakayopambwa na maandamano ya wafanyakazi, maonyesho ya magari ya kazi kutoka taasisi mbalimbali za umma na binafsi.

Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo:
“Upatikanaji wa haki na mazingira bora kazini ni msingi wa uwajibikaji, nidhamu na maadili ya wafanyakazi.”

Kaulimbiu hii inalenga kusisitiza umuhimu wa kuwepo kwa uwiano kati ya haki za wafanyakazi na mazingira bora ya kazi, ili kuimarisha uwajibikaji, nidhamu na kuzingatia maadili katika utekelezaji wa majukumu.

Aidha waziri sharif amertoa wito kwa  wananchi na wafanyakazi kufika Viwanja vya Dole mapema, na  kwa upande wa Wizara, mashirika, taasisi za umma, sekta binafsi na asasi zisizo za kiserikali amezitaka kuratibu usafiri kwa watumishi wao  

Sauti ya Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Sharriff A. Sharriff .