Zenj FM

Dkt. Mwinyi: PBZ ni nguzo ya uchumi wa Zanzibar, yapongezwa kwa miaka 60 ya mafanikio

30 June 2026, 19:31

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi,akizungumza katika maadhimisho ya miaka 60 ya PBZ yaliyofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar.

Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) imeendelea kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya uchumi na kuwataka kuongeza uwekezaji katika huduma za kidijitali ili kuboresha huduma kwa wananchi. Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 60 ya PBZ, ameipongeza benki hiyo kwa mchango wake mkubwa katika ukuaji wa uchumi, ikiwemo kutoa gawio la shilingi bilioni 15.3 kwa Serikali mwaka 2025.

Mary Julus

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) imeendelea kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya uchumi wa Zanzibar, huku akiitaka benki hiyo kuimarisha zaidi huduma zake za kidijitali na kuendelea kuwa chaguo la kwanza kwa wananchi.

Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 60 ya PBZ yaliyofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar, Dkt. Mwinyi amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita sekta ya fedha imeendelea kuwa mhimili wa ukuaji wa uchumi wa Zanzibar, ambapo PBZ imechangia kwa kiasi kikubwa kupitia huduma za kifedha zinazowezesha wananchi kuwekeza, kukuza biashara na kuinua maisha yao.

Rais amesema Serikali inajivunia mafanikio ya PBZ, akieleza kuwa benki hiyo iliyoanzishwa baada ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa lengo la kuwapatia wananchi huduma za kifedha, imeendelea kukua na kuwa moja ya uwekezaji wenye mafanikio makubwa wa Serikali kutokana na uongozi madhubuti na usimamizi bora.

Aidha, amesema jambo linalotia moyo ni PBZ kuendelea kupata tuzo mbalimbali, ikiwemo kupitia programu ya Sema na Rais, pamoja na kuchangia gawio la shilingi bilioni 15.3 kwa Serikali kwa mwaka 2025, jambo alilosema linaonesha uimara wa benki hiyo na mchango wake katika uchumi wa taifa.

Dkt. Mwinyi ameipongeza PBZ kwa kuendelea kuwekeza katika mifumo ya kidijitali na kusisitiza umuhimu wa kuongeza uwekezaji katika teknolojia ili kuboresha huduma kwa wateja na kuendana na kasi ya maendeleo ya sekta ya fedha duniani.

Amesema maadhimisho ya miaka 60 yanapaswa kuwa fursa ya kujitathmini na kupanga dira ya miaka 10 hadi 20 ijayo, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha mtaji, kupanua huduma za kifedha, kuendeleza mifumo ya kidijitali pamoja na kuwawezesha vijana na wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi.

Aidha Rais dkt Mwinyi amewapongeza viongozi wote walioweka msingi wa mafanikio ya PBZ tangu kuanzishwa kwake, pamoja na Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na wafanyakazi kwa mchango wao ulioiwezesha benki hiyo kufikia miaka 60 ya mafanikio.

Sauti ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi,

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa PBZ Juma Hassan Reli amesema maadhimisho hayo ni fursa ya kutambua mchango wa viongozi mbalimbali, marais waliopita na wafanyakazi walioijenga benki hiyo kwa kipindi cha miaka 60.

Sauti ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa PBZ Juma Hassan Reli.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa PBZ CPA Fahad Soud Hamid amesema benki hiyo iliyoanzishwa mwaka 1966 sasa ni miongoni mwa benki sita kubwa nchini Tanzania ikiwa na mtaji unaokadiriwa kufikia zaidi ya shilingi trilioni tatu.

Amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa Serikali, Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na wafanyakazi pamoja na utekelezaji wa mipango ya kimkakati.

Aidha CPA Fahad Amesema PBZ itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar na Tanzania kwa kupanua huduma za kifedha, kuwekeza zaidi katika teknolojia na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa na huduma za kisasa za benki.

Sauti ya Mkurugenzi Mtendaji wa PBZ CPA Fahad Soud Hamid

Top of Form