Zenj FM

Watoto Zanzibar wadai sheria imara kulinda haki zao

24 May 2026, 21:27

Mratibu wa Jukwaa la Watetezi wa Haki za Binadamu Zanzibar, Suleimani Baitan akimkabidhi Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Siti Abasi Ali,maoni na mapendekezo kutoka kwa mabaraza ya watoto huku Mwenyekiti na Makamo Mwenyekiti wakishuhudia tukio hilo.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Siti Abasi Ali, amesema serikali inaendelea kuboresha Sheria ya Mtoto ili kuhakikisha watoto wanaishi katika mazingira salama na yenye ulinzi bora.Watoto kupitia mabaraza yao ya Unguja na Pemba wamewasilisha mapendekezo muhimu kuhusu usalama wa kidigitali, elimu na haki za watoto kusikilizwa katika mashauri yanayowahusu.

Na Mary Julius,

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Siti Abasi Ali, amesema dhamira ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ni kuhakikisha watoto wanaishi katika mazingira salama, yenye ulinzi na yanayowajali.

Amesema watoto hawawezi kulindwa ipasavyo iwapo Sheria ya Mtoto haitakuwa na vifungu madhubuti vinavyozingatia mahitaji na maslahi yao kwa uwazi na ufanisi.

Mkurugenzi Siti ameyasema hayo wakati wa kupokea maoni na mapendekezo kutoka kwa mabaraza ya watoto ya shehia za Unguja na Pemba, ikiwa ni sehemu ya mchakato wa marekebisho ya baadhi ya vifungu vya Sheria ya Mtoto ya Zanzibar.

Amesema ana matumaini kuwa maoni yaliyotolewa yatazingatiwa ili kuhakikisha sheria hiyo mpya inakuwa bora, yenye tija na inayogusa moja kwa moja maisha ya watoto.

Aidha, ameipongeza ZCRF kwa kuendelea kutetea haki za watoto kupitia mabaraza ya watoto, hatua inayosaidia kuibua changamoto zinazowakabili watoto katika jamii.

Sauti ya Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Siti Abasi Ali.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Watoto Zanzibar, Muhsini Haji Simai, ameiomba serikali kuhakikisha sera zinazotungwa zinatekelezwa kwa vitendo pamoja na kuyafanyia kazi mapendekezo ya watoto.

Sauti ya Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Watoto Zanzibar, Muhsini Haji Simai.

Naye Mratibu wa Jukwaa la Watetezi wa Haki za Binadamu Zanzibar, Suleimani Baitan, amesema wadau wa watoto wamewasilisha hoja 16, huku hoja tano zikipewa kipaumbele maalum.

Amesema hoja hizo zinahusu usalama wa kidigitali kwa watoto, elimu, usikilizwaji wa mashauri ya watoto pamoja na maeneo yanayohitaji marekebisho katika sheria iliyopo ili kuendana na mahitaji ya sasa ya jamii.

Sauti ya Mratibu wa Jukwaa la Watetezi wa Haki za Binadamu Zanzibar, Suleimani Baitan.

Kikao hicho kimeandaliwa na Jukwaa la Haki za Watoto Zanzibar kwa kushirikiana na Save the Children na kufanyika katika Ofisi ya Mufti Zanzibar.