Zenj FM
Zenj FM
19 May 2026, 23:50

Kamishna wa Polisi Zanzibar, Kombo Khamis Kombo amewataka askari kufanya kazi kwa weledi, nidhamu na kulinda haki za binadamu pamoja na kushiriki elimu ya Polisi jamii. Aidha amesisitiza matumizi ya mifumo ya TEHAMA na doria kwenye mitandao ya kijamii ili kudhibiti taarifa za uongo zinazoweza kuleta taharuki.
Na Mary Julius.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, CP Kombo Khamis Kombo amesema mafunzo kwa askari ni muhimu ili kuhakikisha wanapandishwa vyeo kwa wakati na kuongeza ufanisi wa kazi.
Akifunga mafunzo ya uongozi mdogo ngazi ya Sajenti Kozi Na. 2/2025–2026 katika viwanja vya Polisi Ziwani Zanzibar, Kamishna Kombo amesema ameridhia kuwatunuku vyeti wahitimu wote waliofaulu mafunzo hayo.
Amewataka askari kufanya kazi kwa weledi, ubunifu na nidhamu, huku wakilinda haki za binadamu na kushiriki kutoa elimu ya polisi jamii. Pia amesisitiza umuhimu wa kuimarisha afya kupitia mazoezi, kupunguza ajali za barabarani, kuharakisha uchunguzi wa kesi za jinai na kudhibiti ukatili wa kijinsia.
Kamishna Kombo amesema Jeshi la Polisi linapaswa kuendelea kutumia mifumo ya TEHAMA na kufanya doria katika mitandao ya kijamii ili kudhibiti usambazaji wa taarifa za uongo zinazoweza kuleta taharuki.
Aidha, amemshukuru Rais wa jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha Jeshi la Polisi kupitia miundombinu, ajira mpya na upandishwaji wa vyeo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Polisi Zanzibar, Moses Neckemia Fundi amesema askari 779 kati ya 781 walifaulu mafunzo yaliyodumu kwa wiki 11 yakihusisha washiriki kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Aidha Amesema changamoto zilizojitokeza ni uchakavu wa majengo, uhaba wa madarasa, vitanda na ghala la kuhifadhia silaha.
Kwa upande wao baadhi ya askali walio maliza mafunzo hayo wameahidi kuyafanyia kazi ili kuongeza ufanisi katika Jeshi la Polisi