Zenj FM
Zenj FM
8 June 2026, 19:01

Baadhi ya wanufaika wa mradi wa utoaji wa miguu bandia Zanzibar wamewataka watu wenye ulemavu wa miguu kujitokeza kwa wingi kupata huduma hiyo muhimu. Miguu hiyo inatolewa kupitia mradi wa Zanzibar 100 Limb Project unaolenga kuwasaidia wananchi 100 kurejea katika maisha yao ya kawaida.
Na Mary Julius.
Baadhi ya wananchi wanaonufaika na zoezi la utoaji wa miguu bandia Zanzibar wamewataka watu wenye ulemavu wa miguu kujitokeza kwa wingi ili kunufaika na huduma hiyo muhimu inayolenga kurejesha matumaini na kuboresha maisha yao.
Wito huo wameutoa leo ikiwa ni siku ya pili tangu kuanza kwa zoezi hilo, mara baada ya kufanyiwa vipimo na kuanza kuchongewa miguu bandia kupitia mradi wa Zanzibar 100 Limb Project, unaotekelezwa na Zanzibar Global Health and Education Foundation kwa ushirikiano na Naya Qadam Trust.
Wanufaika hao wamesema mradi huo ni fursa adhimu kwa watu waliokatwa miguu kwani unawawezesha kurejea katika maisha ya kawaida, kushiriki shughuli za kijamii na kiuchumi pamoja na kujitegemea zaidi.
Aidha, wameishukuru taasisi hiyo kwa msaada walioupata, wakieleza kuwa umewarejeshea imani na matumaini mapya ya maisha.
Kwa upande wake, Mratibu wa kambi hiyo, Othman Ganga Ramadhani, amesema lengo la mradi huo ni kutoa miguu bandia bure kwa wananchi 100 wenye ulemavu wa miguu katika kipindi cha mwezi mmoja, ili kuwawezesha kurejea katika shughuli zao za kila siku na kuongeza ushiriki wao katika maendeleo ya jamii.
Aidha, ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuweka mazingira wezeshi yaliyofanikisha utekelezaji wa zoezi hilo, na kuwataka wananchi wote wanaohitaji huduma ya miguu bandia kufika katika Hospitali ya Mbuzini ili kupata huduma hiyo bila malipo.
Naye Mkuu wa Huduma kwa Wateja wa Seifee Hospital Zanzibar, Antisara Abdalla Salum, amesema uongozi wa hospitali hiyo umejitoa kikamilifu kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa kwa kutoa ushirikiano wa hali ya juu na kuweka mazingira rafiki yatakayowezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi na kwa wakati.
Bottom of Form