Zenj FM

Uzembe wa dereva waua mwanafunzi, mwingine ajeruhiwa Kusini Unguja

29 April 2026, 9:12 pm

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Daniel Emanuel Shillah

Dereva mmoja anashikiliwa na Polisi Mkoa wa Kusini Unguja kwa tuhuma za kusababisha ajali mbaya katika eneo la Mtule. Ajali hiyo ilihusisha gari la abiria lililowagonga watoto wawili waliokuwa wakivuka barabara.

Na Mary Julius.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja linathibitisha kumshikilia dereva mmoja kwa tuhuma za kuendesha gari kwa uzembe na kusababisha ajali iliyopelekea kifo cha mwanafunzi mmoja na kujeruhi mwingine.

Akizungumza na Zenji FM kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Daniel Emanuel Shillah, amesema ajali hiyo ilitokea leo tarehe 29 mwezi wa anne katika eneo la Mtule, Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja.

Kwa mujibu wa Kamanda Shillah, gari la abiria aina ya Toyota Dyna lenye namba za usajili Z 548 LQ, lililokuwa likiendeshwa na Fadhili Kombo Juma, mkazi wa Unguja Ukuu, lilikuwa likitokea Kitogani kuelekea Paje. Dereva huyo alipofika katika eneo la Mtule, aliwagonga watoto wawili waliokuwa wakivuka barabara kwa miguu.

Watoto hao wametambulika kuwa ni Hassan Abdalla Salehe (miaka 11), mwanafunzi wa darasa la tano katika Skuli ya Kitogani, pamoja na Iddi Juma Gwali (miaka 9), mwanafunzi wa darasa la tatu.

Kutokana na ajali hiyo, mwanafunzi Hassan Abdalla Salehe amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Kitogani baada ya kupata majeraha makubwa. Aidha, mwanafunzi Iddi Juma Gwali anaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo, na hali yake inaendelea vizuri.

Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva, aliyekuwa akiendesha gari bila kuchukua tahadhari stahiki katika eneo la makazi ya watu.

Aidha Kamanda Shillah ametoa wito kwa madereva wote kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuchukua tahadhari wanapoendesha vyombo vya moto, hususan katika maeneo ya makazi ya watu, ili kuepusha ajali zisizo za lazima.

Sauti ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Daniel Emanuel Shillah.