Zenj FM

Serikali na JICA waungana kuimarisha miundombinu ya umeme Zanzibar

4 August 2026, 18:24

Meneja wa ZECO Zanzibar, Haji Haji,akiwa pamoja na Mshauri Mwandamizi wa Idara ya Miradi ya Ruzuku kutoka Shirika la JICA, Sugiyama Shigeru, wakisaini makubaliano ya kuanza utafiti wa uwezekano wa utekelezaji wa mradi wa kupokea na kupoza umeme Dimani.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanza maandalizi ya ujenzi wa Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha Dimani kwa kushirikiana na JICA, kupitia utafiti wa upembuzi yakinifu wa mradi huo. Mradi unalenga kuimarisha upatikanaji wa umeme, hasa katika maeneo ya Fumba na viunga vyake, sambamba na kutekeleza malengo ya Sera ya Nishati ya mwaka 2025.

Mary Julius.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefikia hatua muhimu katika maandalizi ya ujenzi wa Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha Dimani, mradi unaotarajiwa kuimarisha upatikanaji wa umeme na kuchochea maendeleo ya kiuchumi, hususan katika maeneo ya Fumba na viunga vyake.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano ya kuanza utafiti wa uwezekano wa utekelezaji wa mradi huo, iliyofanyika katika Ofisi za Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) Saateni, Mkurugenzi wa Idara ya Nishati na Madini, Saidi Haji Mdungi, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa Kushirikiana na JICA ipo katika hatua ya awali ya upembuzi yakinifu kuelekea ujenzi wa kituo hicho.

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutakuwa sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Nishati ya mwaka 2025, inayolenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, salama na endelevu za umeme.

Ameongeza kuwa mradi huo utasaidia kutimiza malengo ya Serikali ya kuwapatia wananchi wa Zanzibar huduma za uhakika za nishati.

Mdungi amesema ongezeko la makazi na maendeleo ya mji wa Fumba pamoja na miji mingine ya kisasa limeongeza mahitaji ya umeme na kusababisha changamoto ya upungufu wa nishati. Amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha changamoto hiyo inapatiwa ufumbuzi kupitia utekelezaji wa mradi wa kituo cha Dimani.

Aidha, ameliomba Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kushirikiana kwa karibu na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA) ili kuhakikisha mahitaji yote ya mradi yanatekelezwa kwa wakati, hivyo kuruhusu ujenzi kuanza na kukamilika kama ilivyopangwa.

Sauti ya Mkurugenzi wa Idara ya Nishati na Madini, Saidi Haji Mdungi.

Kwa upande wake, Meneja wa ZECO Zanzibar, Haji Haji, amesema kutiwa saini kwa makubaliano hayo ni hatua muhimu ya kuanzisha rasmi maandalizi ya mradi utakaosaidia kupunguza changamoto ya uchakavu wa miundombinu na kuongezeka kwa mahitaji ya umeme katika eneo la Fumba.

Amesema kukamilika kwa kituo hicho kutabadilisha mfumo wa usambazaji wa umeme ambapo badala ya umeme kutoka Dar es Salaam kuelekezwa Mtoni na kisha Fumba, sasa utapokelewa Dimani na kusambazwa moja kwa moja katika maeneo ya Fumba, uwanja wa ndege na maeneo mengine ya karibu, hatua itakayoongeza ufanisi na uhakika wa huduma.

Sauti ya Meneja wa ZECO Zanzibar, Haji Haji,

Naye Mshauri Mwandamizi wa Idara ya Miradi ya Ruzuku kutoka Shirika la JICA, Sugiyama Shigeru, amesema kutiwa saini kwa makubaliano hayo kunaashiria kuanza kwa utafiti wa maandalizi utakaotathmini uwezekano wa utekelezaji wa mradi huo.

Amesema utafiti huo utahusisha tathmini za masuala ya kiufundi, kimazingira, kijamii, kiuchumi, kifedha na kitaasisi kwa ushirikiano wa karibu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wadau mbalimbali.

Aidha Sugiyama amesema JICA itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha miundombinu ya umeme ili kusaidia maendeleo endelevu ya kiuchumi, kuongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme na kukidhi mahitaji yanayoendelea kuongezeka visiwani Zanzibar.

Sauti ya Mwandamizi wa Idara ya Miradi ya Ruzuku kutoka Shirika la JICA, Sugiyama Shigeru.

Utiaji wa  saini hiyo imewakilishwa na Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar ZECO Mhandisi Haji Haji na kwa upande wa Serikali ya Japan Imewakilishwa na Mshauri Mkuu wa Idara ya Miradi Mikubwa Sugiyama Shigeru