Zenj FM
Zenj FM
30 May 2026, 23:42

Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, amewataka washiriki wa mafunzo ya usimamizi wa ubora kutumia maarifa waliyojifunza kuongeza ufanisi wa huduma na kupunguza malalamiko ya wananchi.
Na Mary Julius.
Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dk Amour Suleiman amewataka wataalamu 19 waliohitimu mafunzo ya usimamizi wa ubora wa huduma za afya kutumia elimu waliyoipata kuboresha huduma kwa wananchi na kupunguza malalamiko katika vituo vya afya.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar wakati wa hafla ya utoaji vyeti, iliyo fanyika katika hotel ya Golden Tulip Uwanja wa ndege Zanzibar , Dk Amour amesema ubora wa huduma ni jukumu la kila mfanyakazi wa afya kuanzia mlinzi hadi viongozi wa hospitali.
Amepongeza ushirikiano wa Pharma Access katika kuimarisha sekta ya afya na kuwataka wahitimu kuwa chachu ya mabadiliko.
Aidha amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi imeendelea kuipa kipaumbele sekta ya afya kwa kuongeza bajeti na kuboresha mazingira ya kazi kwa wataalamu wa afya ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wake, Meneja Mradi kutoka Pharm Access Dkt Faiza Abasi amesema mafunzo hayo yataimarisha uwezo wa wataalamu wa afya na kuongeza ufanisi wa huduma kwa wananchi.
Dkt. Faiza amesema Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika ujenzi wa miundombinu ya afya, hivyo ni wajibu wa wahudumu kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zinazostahili. Ameeleza kuwa huduma bora za afya ni haki ya msingi ya kila mwananchi na kwamba mifumo ya kidijitali inayozidi kuimarishwa itasaidia kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma.
Naye Kiongozi wa Kitengo cha Ubora wizara ya Afya Zanzibar Hasfa .M. Haji amesema zaidi ya vituo 300 vya afya vimefanyiwa tathmini ya ubora huku wahitimu hao wakitarajiwa kusaidia kusimamia viwango vya huduma.
Awali, Mkurugenzi Idara ya Uuguzi na Ukunga, Mwanaisha Juma Fakih,, amesema kuongezeka kwa wataalamu hao wa tathmini kutasaidia kuimarisha ubora wa huduma za afya na kupunguza malalamiko ya wananchi Zanzibar.
Kwa upande wao wahitimu wa mafunzo hayo wameahidi kuyafanyia kazi mafunzo hayo ili kuweza kuboresha huduma za afya katika hospital na vituo vya afya.
Aidha wameipongza wizara ya afya Zanzibar na pharmacces kwa kuendelea kuwajengea uwezo wahudumu wa afya .