Zenj FM

Mapambano dhidi ya dhana potofu za chanjo yaendelea Kaskazini A

24 June 2026, 14:39

Kituo cha afya cha Chaani Kikobweni

Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii Wilaya ya Kaskazini A wametajwa kuwa chachu ya mafanikio ya chanjo kwa kuwafikia wananchi nyumba kwa nyumba na kuhakikisha watoto wote wanaostahili wanapata huduma kwa wakati. Hata hivyo, wananchi wametakiwa kuachana na dhana potofu kuhusu chanjo na kuendelea kushirikiana na wataalamu wa afya kulinda afya za watoto na jamii kwa ujumla.

Na Mary Julius.

Mratibu wa Huduma za Afya Ngazi ya Jamii Wilaya ya Kaskazini A, Hafife Ali Mussa, amesema wahudumu wa afya ya jamii wamechangia kwa kiwango kikubwa kuhakikisha wananchi wanaohitaji chanjo wanazipata kwa wakati katika wilaya hiyo.

Amesema hayo wakati wa ziara ya mwandishi wa Zenji FM katika Shehia ya Chaani Kubwa, ambapo ameeleza kuwa wahudumu hao wamekuwa wakipita nyumba kwa nyumba kufuatilia na kuboresha huduma za afya ngazi ya jamii.

Hafidh amesema wahudumu wa afya wamekuwa wakiwatambua na kuwafuatilia akina mama wenye watoto walio katika umri wa kupata chanjo ili kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa huduma hiyo muhimu. Ameongeza kuwa mfumo wa afya ngazi ya jamii umewezesha kutambua watoto waliozaliwa, wajawazito na wazee, jambo linalorahisisha utoaji na usimamizi wa huduma za afya kwa kushirikiana na Wizara ya Afya.

Aidha, amesema wahudumu hao hupita katika mashehia mbalimbali kuwafikia watoto ambao hawajapata chanjo na kuhakikisha wanapatiwa huduma hiyo kwa wakati.

Kwa mujibu wa Hafidh, miongoni mwa mikakati waliyojiwekea ni kushirikiana na ofisi za masheha, skuli pamoja na watu mashuhuri katika jamii ili kuendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa chanjo.

Hata hivyo, amesema bado wanakabiliwa na changamoto ya baadhi ya wananchi kuwa na dhana potofu kuhusu chanjo. Amewataka wananchi kuachana na imani hizo na kuendelea kushirikiana na wataalamu wa afya kwa ajili ya kulinda afya za watoto na jamii kwa ujumla.

Sauti ya Mratibu wa Huduma za Afya Ngazi ya Jamii Wilaya ya Kaskazini A, Hafife Ali Mussa,

Akizungumzia chanjo ya HPV, Hafidh amesema mwaka jana wilaya hiyo ilifanikiwa kufikia asilimia 120 ya lengo la watoto waliotakiwa kuchanjwa. Kwa mwaka huu, wilaya imefikia asilimia 54 ya watoto wenye umri wa miaka tisa wanaostahili kupata chanjo hiyo.

Amefafanua kuwa idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kwani bado watoto wengine hawajafikia umri unaostahili. Amesema wilaya imepanga kuanza kampeni maalumu mwezi Septemba ili kuhakikisha watoto wote wenye sifa wanapatiwa chanjo ya HPV.

Sauti ya Mratibu wa Huduma za Afya Ngazi ya Jamii Wilaya ya Kaskazini A, Hafife Ali Mussa,

Kwa upande wake, Mhudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wa Shehia ya Chaani Kubwa, Zainabu Hassan Simai, amesema amekuwa akitembelea kaya mbalimbali kuwafuatilia watoto wanaostahili kupata chanjo pamoja na wajawazito, huku akihamasisha mahudhurio ya kliniki kufikia mara nane kama inavyoshauriwa na wataalamu wa afya.

Sauti ya Mhudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wa Shehia ya Chaani Kubwa, Zainabu Hassan Simai,

Naye Mariamu Hamadi, mkazi wa Chaani na mama mwenye mtoto wa mwaka mmoja, amesema chanjo ni muhimu kwa watoto kwani huwakinga dhidi ya magonjwa mbalimbali. Amewataka wazazi wengine kutodharau chanjo kutokana na manufaa yake kwa afya ya watoto.

Amina Kombo naye amesema chanjo husaidia kuwalinda watoto dhidi ya maradhi na ulemavu, hivyo jamii inapaswa kuendelea kuitikia wito wa kuwapeleka watoto wao kupata huduma hiyo.

Sauti ya wananchi.

Kwa upande wake, Mratibu wa Afya ya Mama na Mtoto katika Kituo cha Afya Chaani Kubwa, Mariamu Saidi, amesema wananchi wengi wameelewa umuhimu wa chanjo, ingawa bado kuna baadhi wanaohitaji kuendelea kupewa elimu zaidi.

Amesema kituo hicho huendesha huduma za outreach kila mwezi ili kuwafikia watoto wanaoshindwa kufika vituoni kwa ajili ya chanjo. Kuhusu chanjo ya HPV, amesema wahudumu wa afya wamekuwa wakitembelea shule mbalimbali kutoa chanjo hiyo na kuwafikia watoto wengi zaidi.

Aidha, ameiomba Wizara ya Afya kuendelea kutoa usaidizi kwa wahudumu wa afya ya jamii ili kuwawezesha kuwafikia watoto wengi zaidi mashuleni na katika maeneo ya makazi yao.

Sauti ya Mratibu wa Afya ya Mama na Mtoto katika Kituo cha Afya Chaani Kubwa, Mariamu Saidi,