Zenj FM
Zenj FM
2 July 2026, 02:29

Mradi wa Zanzibar 100 Limb Project umefanikiwa kuwafikia watu 94 kati ya 100 waliolengwa, huku watu 88 wakipatiwa miguu bandia, na hivyo kufikia zaidi ya asilimia 90 ya malengo yake.Nao wanufaika na vijana waliopata mafunzo ya utengenezaji wa miguu bandia wamesema mradi huo umeongeza uwezo wa kujitegemea na kuboresha huduma kwa watu wenye uhitaji wa viungo bandia.
Mary Julius.
Mratibu wa Mradi wa Zanzibar 100 Limb Project , El’Jabir Shao, amesema mradi huo umefanikiwa kuwafikia watu 94 kati ya 100 waliolengwa, huku watu 88 wakipatiwa miguu bandia, hatua iliyowezesha kufikiwa kwa zaidi ya asilimia 90 ya malengo ya mradi.
Amesema sababu kuu iliyochangia kutofikiwa kwa lengo la asilimia 100 ni mwamko mdogo wa baadhi ya walengwa kujitokeza kupata huduma hiyo, licha ya juhudi mbalimbali zilizofanyika kuwafikia.
Mradi huo ulilenga kuwapatia watu 100 viungo bandia vya miguu ili kuwawezesha kurejea katika maisha yao ya kawaida na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
El’Jabir Shao ametoa shukrani za dhati kwa Jafferji Family, wakiwemo Javed, Kulsum, Kumail, Zariana na Zera, kwa mchango wao mkubwa wa kifedha na wa kibinadamu uliofanikisha utekelezaji wa mradi huo.
Aidha, ameishukuru Taasisi ya UWZ kwa ushirikiano wake mkubwa katika kuwabaini na kuwafikia watu wenye ulemavu, jambo lililorahisisha utekelezaji wa mradi huo.
Kwa upande wao, wanufaika wa miguu bandia wamesema msaada huo utawarejeshea uwezo wa kutekeleza majukumu yao ya kila siku na kuwapa fursa ya kujitegemea pamoja na kuhudumia familia zao.
Aidha wamesema kupatiwa mguu bandia kutamwezesha kurejea katika shughuli zake za kijamii na kiuchumi, huku wakiwaomba watu wenye uwezo kuendelea kuwasaidia watu wenye ulemavu ili kuboresha maisha yao.
Nao vijana waliopatiwa mafunzo ya kutengeneza miguu bandia, wamesema ujuzi walioupata ni muhimu na utawasaidia kuwahudumia watu wengi zaidi wenye uhitaji wa viungo bandia, baada ya kubaini kuwa mahitaji ya huduma hiyo ni makubwa katika jamii.
Wakizungumzia upatikanaji wa vifaa vya kutengenezea miguu bandia, mmoja wa wakufunzi amesema ubunifu unaotumika unazingatia mazingira yaliyopo, hivyo upatikanaji wa malighafi na vifaa si changamoto kubwa.
Mradi huo ulio anza tarehe moja mwezi wa sita na kukamilika tarehe 1 mwezi wa saba zmbapo huduma hizo zilikuwa zinatolewa katika hospital ya wilaya ya Mbuzini, Wilaya Ya Magharib A.