Zenj FM

Mataifa 12 yathibitisha ushiriki katika tamasha la uwekezaji Zanzibar 2026

2 June 2026, 18:52

Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff,Akizungumza na waandishi wa habari Zanzibar, Waziri wa Kazi na Uwekezaji.

Zanzibar imekamilisha maandalizi ya Tamasha la Uwekezaji Zanzibar 2026 litakalofanyika kuanzia Juni 3 hadi 5, likiwakutanisha wawekezaji, wafanyabiashara na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi. Zaidi ya washiriki 600 kutoka mataifa zaidi ya 12 wamejisajili kushiriki katika tamasha hilo la kimataifa.

Na Mary Julius.

Zanzibar imekamilisha maandalizi yote ya kuwapokea mamia ya wawekezaji, wafanyabiashara na wadau wa maendeleo kutoka mataifa mbalimbali watakaoshiriki Tamasha la Uwekezaji Zanzibar 2026 litakaloanza kesho Juni 3 hadi 5 katika Hoteli ya Golden Tulip Airport Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari Zanzibar, Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff, amesema Serikali ipo tayari kwa tamasha hilo kubwa la kimataifa ambalo linatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kutangaza fursa za uwekezaji na biashara zilizopo Zanzibar.

Waziri Shariff amesema hadi kufungwa rasmi kwa zoezi la usajili, zaidi ya washiriki 600 wamejisajili kushiriki tamasha hilo huku zaidi ya mataifa 12 yakithibitisha kushiriki.

Amesema mwitikio huo mkubwa ni ishara ya kuendelea kuimarika kwa imani ya wawekezaji na wadau wa maendeleo katika mazingira ya uwekezaji na biashara yanayoendelea kuboreshwa Zanzibar.

Waziri Sharif amesema Tamasha la Uwekezaji Zanzibar 2026 litawakutanisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, viongozi wa Serikali, taasisi za fedha, sekta binafsi pamoja na washirika wa maendeleo kwa lengo la kujadili fursa mpya za uwekezaji na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi.

Aidha, amesema tamasha hilo linatarajiwa kufungua milango mipya ya biashara, kuvutia mitaji zaidi na kuongeza mchango wa sekta binafsi katika ukuaji wa uchumi na utoaji wa ajira kwa wananchi.

Sauti ya Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff.