Talaka chanzo cha matatizo ya afya ya akili kwa wanawake na watoto Zanzibar
10 October 2024, 5:27 pm
Kwa mujibu wa ripoti ya afya ya akili duniani ya 2022 inasema takribani Mtu mmoja kati kila watu manne wanaugua aina moja ya ugonjwa Unaohusiana na afya ya akili.
Na Mwanamiraji Abdallah.
Mkuu wa Divisini ya Afya ya Akili Inayo Simamiwa na Hospital ya Mnazimmoja Ambaye Pia ni Daktari Bingwa Wa Afya Ya Akili Hospital Ya Kidongo Chekundu Dk Khadija Abdulrahman amesema chanzo cha matatizo ya afya ya akili kwa upande wa wanawake ni kuongezeka kwa talaka.
Akizungumza na waaandishi wa habari katika maadhimisho ya siku ya afya ya akili duniani katika viwanja vya mapinduzi square. amesema ndoa ambazo hazina utulivu hupelekea talaka ambazo zimekuwa zikiwaathiri wanawake wengi visiwani Zanzibar kwani wengi wao ni tegemezi hali inayopelekea kupata msongo wa mawazo.
Kwa upande wa wanaume Dk Khadija amesema kukosekana kwa malezi bora kwa watoto ndio kumepelekea vijana wengi kujiingiza katika matumizi ya madawa ya kulevya na kuwa awaadhirika wakubwa wa matatizo ya afya ya akili.
Mkuu Wa Kitengo Cha Matibabu ya Afya ya Akili Hospitali Ya Kidongo Chekundu Maryam Saleh Sultan amesema kuwa wagonjwa wa afya ya akili wanatakiwa kupewa matibabu bora na kipaumbele zaidi katika jamii kwani na wao wanauwezo wa kufanya mambo mazuri mbali mbali katika jamii yao.
Kwa upande wake Mratibu wa Afya ya Akili Hamida Naufal Kassim amesema kwanzia kipindi cha july 2023 mpaka june 2024 wagonjwa wa afya ya akili walio hudhulia katika hospital ya Kidongo chekundu ni 3611.