Zenj FM
Zenj FM
26 April 2026, 9:48 pm

Zanzibar itaadhimisha Siku ya Usalama na Afya Kazini kupitia kongamano maalum litakalofanyika Aprili 28. Mjadala mkuu utazingatia changamoto za msongo wa mawazo na afya ya akili kazini kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza tija sehemu za kazi.
Na Mary Julius
Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Sharif Ali Sharif, amesema msongo wa mawazo kazini bado ni changamoto kubwa inayowakumba wafanyakazi wengi nchini, ambapo tafiti zinaonesha kuwa takribani asilimia 61 ya wafanyakazi hupitia hali hiyo, jambo linaloathiri tija na kuchochea migogoro sehemu za kazi.
Waziri Sharif ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari,katika ukumbi wa ofisi hiyo Mwanakwerekwe mkoa wa Mjini Magharib , waziri amesema katika kuadhimisha Siku ya Usalama na Afya Kazini (OSH) tarehe 28 Aprili, Zanzibar itafanya kongamano maalum litakalowakutanisha wadau kutoka sekta za umma na binafsi.
Waziri amesema kaulimbiu ya mwaka huu ni “Mazingira bora ya kazi kisaikolojia na kijamii ni njia ya kuimarisha ustawi wa wafanyakazi na kujenga taasisi imara” inalenga kuhimiza umuhimu wa kushughulikia hatari za kisaikolojia mahali pa kazi na kuimarisha afya ya akili ya wafanyakazi.
Ameongeza kuwa mfanyakazi mwenye afya njema na anayejihisi kuthaminiwa hufanya kazi kwa ufanisi zaidi, hivyo kuchangia moja kwa moja katika maendeleo ya taasisi na taifa kwa ujumla.
Amesisitiza kuwa ustawi wa mfanyakazi ni nguzo muhimu katika mafanikio ya taasisi yoyote, huku Wizara ya Kazi kupitia Idara ya Usalama Kazini ikiendelea kuimarisha mikakati ya kuboresha mazingira ya kazi nchini.
Aidha, ametoa wito kwa wafanyakazi kujali afya zao kwa kufanya mazoezi na kupata mapumziko ya kutosha, huku akiwataka waajiri kutoa msaada wa kisaikolojia na kuepuka ratiba zenye shinikizo kubwa zinazoweza kuathiri afya ya wafanyakazi.
Mgeni rasmi katika kongamano hilo anatarajiwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla ambapo mada mbili zitawakilishwa.