Zenj FM
Zenj FM
24 July 2026, 13:50

Kikundi cha Wanawake Wenye Ulemavu Kusini Unguja (WUKU) kimesema mradi unaofadhiliwa na ADD umewawezesha wanachama kuimarisha shughuli zao za kiuchumi kupitia mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya fedha. WUKU imeahidi kuendeleza mafanikio hayo kwa kushirikiana na ADD na UWZ ili kuwainua zaidi wanawake na wasichana wenye ulemavu.
N a Mary Julius.
Mratibu wa Kikundi cha Wanawake Wenye Ulemavu Kusini Unguja (WUKU), Khairoun Mambo, amesema kikundi hicho kimepata mafanikio makubwa kupitia mradi unaofadhiliwa na ADD, uliowajengea wanachama uwezo wa kuimarisha shughuli zao za kiuchumi.
Khairoun amesema baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi, wanachama wameonyesha maendeleo makubwa na sasa wanaendelea kujipanga kuhakikisha mafanikio hayo yanaendelezwa katika awamu zinazofuata.
Ameeleza kuwa tarehe 21 Julai, WUKU ilipokea ugeni kutoka ADD uliolenga kuimarisha ushirikiano kati ya wafadhili na wanufaika wa mradi. Ziara hiyo pia ilitoa nafasi ya kutathmini mafanikio yaliyofikiwa, kubaini changamoto zilizopo na kujadili maboresho yatakayotekelezwa kabla ya kuanza awamu mpya ya mradi.
Akizungumza na Zenj FM, Khairoun amesema lengo la ziara hiyo ni kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya ADD, UWZ na WUKU, sambamba na kuboresha utekelezaji wa mradi kwa manufaa ya wanawake na wasichana wenye ulemavu.
Amesema matarajio yao ni kuunda vikundi zaidi vya kiuchumi, kutoa mafunzo ya ujasiriamali, elimu ya fedha na kuwajengea wanachama uwezo wa kupata mikopo ili kuongeza uzalishaji na kujitegemea kiuchumi.
Kwa upande wake, Donald Naveta amesema UWZ inaendelea kusimamia fedha za mradi kwa niaba ya WUKU kutokana na kukosekana kwa mtaalamu wa usimamizi wa fedha ndani ya kikundi hicho.
Amesema fedha hizo hutolewa kwa kuzingatia mpango mkakati uliowekwa ili kuhakikisha zinatumika kwa uwazi, ufanisi na kwa malengo yaliyokusudiwa.
Aidha, amewahimiza wanachama wa WUKU kutumia kikamilifu maarifa waliyojifunza kupitia mradi huo na kuongeza juhudi katika shughuli za uzalishaji mali ili kufikia maendeleo endelevu.
Naye mmoja wa wanachama wa WUKU amesema mafunzo waliyopata yamewawezesha kujiimarisha kiuchumi, kufahamu haki zao na kushiriki kikamilifu katika kuzitetea kwa kushirikiana na uongozi wa UWZ.