Zenj FM
Zenj FM
13 September 2026, 23:12

Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji, Shaaban Ali Othman, ameitaka ZEEA kuwafuata wajasiriamali katika maeneo yao ya biashara na kutatua changamoto zinazowakabili. Amesema huduma za uwezeshaji, ikiwemo mikopo na elimu ya biashara, zinapaswa kuwafikia wananchi kwa vitendo ili kukuza biashara na kuongeza ajira. Waziri Shaaban ametoa kauli hiyo wakati akifunga Tamasha la Fahari ya Zanzibar katika viwanja vya Mnazimmoja.
Na Mary Julius
Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji, Shaaban Ali Othman, ameitaka Mamlaka ya Uwezeshaji Zanzibar ZEEA kubadilisha mfumo wa kuwahudumia wajasiriamali kwa kuwafuata moja kwa moja katika maeneo yao ya biashara na kutatua changamoto zinazowakabili.
Waziri Shaaban amesema hayo wakati akifunga Tamasha la Fahari ya Zanzibar katika viwanja vya Mnazimmoja, amesema uwezeshaji wa wananchi haupaswi kusubiri viongozi wafike katika maeneo yao ndipo changamoto zibainike.
Waziri Shaaban amesema ZEEA inapaswa kuhakikisha huduma za uwezeshaji, ikiwemo mikopo, elimu ya biashara na fursa mbalimbali, zinawafikia wananchi kwa vitendo.
Ameitaka ZEEA kuanza mara moja ziara kwa wafanyabiashara katika maeneo yao, kusikiliza changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi, ili kuweka mazingira bora ya kukuza biashara na kuongeza ajira.
Aidha, Waziri Shaaban ameiagiza ZEEA kufanya tathmini ya Tamasha la Fahari ya Zanzibar, kubaini mafanikio na changamoto zilizojitokeza na kutumia matokeo hayo katika kuboresha matamasha yajayo.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa TANTRADE Zanzibar, Fred Liundi, amesema tamasha hilo limeiwezesha TANTRADE kukutana moja kwa moja na wazalishaji na wajasiriamali, kusikiliza mahitaji yao na kuwaunganisha na fursa za biashara pamoja na masoko.
Fred amesema TANTRADE itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ZEEA na wadau wengine katika kuwawezesha wajasiriamali, huku akiwataka wananchi kuunga mkono bidhaa zinazozalishwa nchini.
Amesema miongoni mwa elimu iliyotolewa katika tamasha hilo ni matumizi ya nembo ya Made in Tanzania, akieleza kuwa elimu hiyo ni muhimu kwa wajasiriamali katika kuitangaza na kuitambulisha bidhaa yao katika masoko.
Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya TANTRADE na ZEEA umefikia mwaka wa tatu mfululizo, kupitia makubaliano maalum yenye lengo la kukuza biashara za Tanzania, hususan biashara za wajasiriamali.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ZEEA, Juma Burhan Mohamed, amesema Tamasha la Fahari ya Zanzibar, lenye kaulimbiu “Bidhaa Zetu Ndio Fahari Yetu,” limewapa wanawake, vijana na wajasiriamali fursa ya kuonesha bidhaa, vipaji na ubunifu wao pamoja na kutafuta masoko.
Juma amesema uwezeshaji wa kweli hauishii katika kutoa mtaji pekee, bali unahusisha pia maarifa, teknolojia, uzalishaji bora na upatikanaji wa masoko ambapo ushiriki wa TANTRADE umewezesha washiri wa tamasha hilo kupata elimu zote hizo.
Amesema ZEEA na TANTRADE zitaendelea kutekeleza makubaliano yao ya ushirikiano kwa lengo la kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi, hususan wajasiriamali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Vijana Zanzibar, Mohamed Abraham Juma, amesema lengo kuu la Tamasha la Fahari ya Zanzibar ni kuwaonesha vijana fursa mbalimbali zinazoweza kuwawezesha kujiajiri na kujenga maisha yao.
Mohamed ameipongeza TANTRADE kwa kuandaa tamasha hilo na kuwataka vijana kutotazama fursa kama watazamaji, bali kuzitumia kujenga ajira na kuendeleza vipaji pamoja na ubunifu wao.