Zenj FM
Zenj FM
1 October 2026, 12:21

Mafunzo ya siku tatu yamewajengea uwezo washiriki 49 kutoka Unguja katika ukusanyaji, utunzaji na matumizi ya taarifa kwa ajili ya kuimarisha huduma usaidizi wa sheria Unguja.
Na Mary Julius.
Jumuiya za wasaidizi wa sheria zimetakiwa kuweka na kutumia ipasavyo data wanazokusanya, ili kusaidia Serikali katika kupanga na kuboresha huduma za kisheria kwa wananchi.
Akizungumza pembezoni mwa kikao cha siku tatu cha kuwajengea uwezo wasaidizi wa sheria kuhusu utunzaji wa data pamoja na Ufuatiliaji na Tathmini, Afisa wa Ufuatiliaji wa Tathmini kutoka Enabel, Essau Amenye, amesema taarifa hizo ni muhimu katika kufuatilia idadi ya wananchi wanaofikiwa na huduma za wasaidizi wa sheria.
Amesema matumizi sahihi ya data yanawezesha kutathmini mafanikio ya huduma zinazotolewa, pamoja na kubaini maeneo yanayohitaji kupewa kipaumbele.
Amesema mafunzo hayo yataonyesha uhusiano wa tasisi za serikali na jumuiya za wasaidizi wa sheria pamoja na mchango wa kuanzia ngazi ya chini, nakujua jamii inanufaika vip na uwepo wa jumuiya za wasaidizi wa kisheria.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mtandao wa Jumuiya za Wasaidizi wa Sheria Zanzibar, ZAPONET, Asia A. Hussein, amesema mafunzo hayo yamedhaminiwa na Enabel kupitia mradi wa Sauti ya Mwanamke, amesema mafunzo hayo pia yamelenga kuwajengea uwezo wasaidizi wa sheria katika kufuatilia kesi wanazowasaidia wananchi hadi zinapofikia hatua ya kupata maamuzi katika mahakama au mabaraza ya sheria.
Asia amesema mafunzo hayo yameshirikisha washiriki 49 kutoka Unguja, huku yakitarajiwa kufanyika pia Pemba kwa kuwashirikisha jumuiya za wasaidizi wa sheria za kisiwa hicho.
Kwa upande wao, baadhi ya wasaidizi wa sheria walioshiriki mafunzo hayo wameushukuru uongozi wa ZAPONET pamoja na Enabel kwa kuwawezesha kupata mafunzo hayo.
Wamesema awali walikuwa wakikabiliwa na changamoto katika kujaza fomu na kuandaa ripoti, lakini mafunzo hayo yamewasaidia kuongeza uelewa na ujuzi katika maeneo hayo.
Wameomba wafadhili kuendelea kuwaunga mkono kwa kuwapatia mafunzo zaidi, huku wakiahidi kutumia ujuzi walioupata kuwaelimisha wasaidizi wengine katika jumuiya zao.