Zenj FM
Zenj FM
24 November 2026, 16:29

Wananchi wa Wilaya ya Kati wametakiwa kuzingatia masharti ya mikopo ya asilimia 4, 4 na 2 inayotolewa na Serikali kupitia ZEEA ili kunufaika na fursa hiyo ya kujikwamua kiuchumi.
Na Wilaya ya Kati.
Wananchi wa Wilaya ya Kati wametakiwa kuzingatia miongozo na masharti ya mikopo ya asilimia 4,4,2 inayotolewa na Serikali kupitia Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo hiyo.
Wito huo umetolewa na Afisa Mikopo wa ZEEA, Yusra Hemed Mkumbaru, katika mkutano wa kutoa elimu ya utaratibu wa mikopo hiyo uliofanyika Baraza la Manispaa Kati, Dunga.
Amesema elimu hiyo inalenga kuwajengea uwezo watendaji wa Manispaa kusimamia utoaji wa mikopo na kuhamasisha vikundi vya ujasiriamali kujiunga na kunufaika na fursa hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Kati, Dkt. Mwanaisha Ali Said, amesema Manispaa itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu taratibu za kuomba mikopo na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuomba mikopo hiyo ili kujikwamua kiuchumi.
Naye Mkuu wa Divisheni ya Mapato, Uchumi na Wajasiriamali wa Manispaa hiyo, Mussa Abdurab Fadhili, amesema mikopo hiyo inatolewa kwa kuzingatia miongozo maalumu ya Serikali.
Nao baadhi ya washiriki wamewahimiza wanawake kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali ili kuongeza kipato na kuboresha maisha ya familia zao.
Mkutano huo umewashirikisha watendaji, maafisa wanaosimamia wajasiriamali pamoja na wawakilishi wa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu Wilaya ya Kati.