Zenj FM
Zenj FM
15 November 2026, 00:07

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Dk. Nasra Nassor Omar, ameitaka sekta binafsi kutumia fursa na miundombinu ya Serikali kuboresha huduma na kuongeza ushindani wa utalii. Wakati huo huo, wadau wa utalii wametaka udhibiti wa vishoka na kuimarishwa kwa usalama wa wageni ili kukuza sekta hiyo.
Na Mary Julis
Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Dk. Nasra Nassor Omar, ameitaka sekta binafsi ya utalii kupitia Chama cha Waendesha Shughuli za Utalii Zanzibar (ZATO), kutumia fursa na miundombinu inayowekwa na Serikali kuimarisha huduma, kuongeza ushindani na kukuza utalii wa Zanzibar.
Akizungumza katika Jukwaa la Wadau wa Utalii (ZATO Stakeholders Forum), lililofanyika Hoteli ya Verde Zanzibar, Dk. Nasra amesema ZATO ina wajibu wa kuwakilisha maslahi ya wanachama wake, kuimarisha weledi na kuhakikisha watoa huduma za utalii wanazingatia maadili ya kitaaluma, sheria na viwango vinavyotakiwa.
Amesema Serikali inaendelea kuweka miundombinu na mazingira wezeshi kwa ajili ya kukuza sekta ya utalii, hivyo ni wajibu wa ZATO na wadau wengine kuitumia fursa hiyo ipasavyo kwa kuwekeza,ili kuboresha huduma na kuongeza mchango wao katika uchumi wa Zanzibar.
Waziri Nasra ameipongeza ZATO kwa kuandaa jukwaa hilo, akieleza kuwa ni fursa muhimu kwa wadau kutafakari walikotoka, walipo na wanakokwenda katika kuendeleza sekta ya utalii.
Aidha, amesema Serikali inahitaji sekta binafsi yenye ubunifu, uwekezaji na uwezo wa kushindana katika soko la kimataifa, huku akisisitiza umuhimu wa usimamizi madhubuti na ushirikiano kati ya taasisi za Serikali na wadau.
Akizungumzia kaulimbiu ya jukwaa hilo, Digital, Inclusive and Sustainable Tourism of Zanzibar, amesema matumizi ya teknolojia, utalii jumuishi na endelevu ni mambo muhimu katika kuongeza ushindani na kuhakikisha fursa za utalii zinawanufaisha vijana, wanawake, wajasiriamali wadogo na jamii zinazozunguka vivutio vya utalii.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ZATO, Aisha Hussein Mussa, amesema mafanikio ya sekta ya utalii yanapaswa kupimwa pia kwa namna yanavyoboresha maisha ya wananchi na kuwapatia wageni wanaotembelea Zanzibar kumbukumbu nzuri.
Ameiomba Serikali kuimarisha usimamizi wa shughuli za utalii kwa kuweka mifumo na taratibu madhubuti kwa taasisi zinazohusika, ili kuhakikisha ushindani wa haki, uhalali wa watoa huduma na viwango vinavyolinda wageni.
Aisha amesema ZATO itaendelea kujenga uwezo wa wanachama wake, kuimarisha weledi na kupanua ushirikiano na wadau mbalimbali, huku ikiwa tayari kutoa utaalamu na kushiriki katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazoikabili sekta hiyo.
Nao washiriki wa jukwaa hilo wamesema jukwaa hilo limelenga kujadili namna ya kuendeleza utalii kupitia mifumo ya kidijitali, kuboresha mazingira ya utendaji kazi na kuweka maazimio yatakayowasilishwa kwa viongozi wa Serikali kwa ajili ya kushughulikia changamoto za wadau.
wamesema miongoni mwa changamoto zinazohitaji ufumbuzi ni uwepo wa watu wanaojihusisha na shughuli za utalii nje ya mifumo na taratibu rasmi, maarufu kama vishoka, hali inayoweza kuathiri ushindani na mazingira ya biashara kwa watoa huduma wanaofuata sheria.
Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Utalii Zanzibar, Luteni Kanali Majaliwa Adam Waziri, amesema Kikosi cha Polisi Utalii kimeundwa kwa lengo la kuhakikisha usalama wa wageni tangu wanapoingia Zanzibar hadi wanapoondoka kurejea katika nchi zao.
Aidha Amewaomba wadau wote wa utalii kutoa ushirikiano wa dhati kwa Polisi Utalii ili kuwezesha kikosi hicho kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuhakikisha wageni wanaotembelea Zanzibar wanapata usalama na huduma zinazostahili.