Zenj FM
Zenj FM
27 November 2026, 13:21

Afisa Afya wa Wilaya ya Magharibi A, Faiza Mohammed, amewataka wazazi na skuli binafsi kuhakikisha watoto wenye umri wa miaka tisa wanapata chanjo ya HPV kwa wakati ili kujikinga na saratani ya mlango wa kizazi.
Afisa Afya wa Wilaya ya Magharibi A, Faiza Mohammed, amewaomba wazazi kuhakikisha watoto wenye umri wa miaka tisa wanapata chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi (HPV) kwa wakati ili kujikinga na ugonjwa huo.
Akizungumza na mwandishi wa Zenj FM aliyemtembelea ofisini kwake, Faiza amesema wilaya hiyo imepata mafanikio katika utoaji wa chanjo mbalimbali kwa mwaka 2026, ambapo watoto 8,647 wamepatiwa chanjo, sawa na asilimia 84, huku watoto 4,922 wakipata chanjo ya HPV, sawa na asilimia 100 ya lengo lililowekwa.
Aidha, amesema wajawazito 9,131 wamepatiwa chanjo mbalimbali, sawa na asilimia 58, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha afya ya mama na mtoto.
Hata hivyo, amesema changamoto ya uelewa miongoni mwa baadhi ya wazazi kuhusu chanjo ya HPV imeendelea kushughulikiwa kupitia utoaji wa elimu katika mikutano ya jamii na wahudumu wa afya wanaofika nyumba kwa nyumba.
Katika hatua nyingine, amezitaka skuli binafsi kushirikiana na maafisa afya kuhakikisha watoto wote wenye umri wa miaka tisa wanapata chanjo hiyo kwa wakati.