Zenj FM
Zenj FM
5 September 2026, 17:41

Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itaendelea kuimarisha uwezeshaji wa wananchi kwa kuongeza upatikanaji wa mitaji, kuimarisha Mfuko wa Uwezeshaji na kukuza miradi ya kuongeza thamani ya bidhaa. Kauli hiyo imetolewa wakati wa Tamasha la Tatu la Fahari ya Zanzibar 2026, lililowakutanisha serikali, sekta binafsi, taasisi za fedha na wajasiriamali. Aidha, Stanbic Bank Tanzania na ZEEA zimesaini makubaliano ya miaka mitano ya kukuza ujasiriamali, huduma za kifedha na biashara endelevu Zanzibar.
Na Mary Julius
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itaendelea kuipa kipaumbele ajenda ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa kuongeza upatikanaji wa mitaji, kuimarisha Mfuko wa Uwezeshaji, kuongeza wataalamu pamoja na kuendeleza miradi ya kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa Zanzibar.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo katika uzinduzi wa Tamasha la Tatu la Fahari ya Zanzibar 2026, katika Hotuba ya yake ilisomwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, ambaye alimwakilisha Rais katika ufunguzi wa tamasha hilo. lililofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Serikali inalenga kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi hauishii kwenye takwimu pekee, bali unaonekana moja kwa moja katika maisha ya wananchi kupitia ajira, kipato, fursa za biashara na kuongezeka kwa ustawi wa jamii.
Aidha, Hemed ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kutoa kipaumbele katika masuala ya uwezeshaji wakati wa kupanga ukomo wa bajeti za Serikali, pamoja na kuhakikisha fedha zilizoidhinishwa zinaingizwa kwa wakati katika taasisi zinazohusika.
Aidha ameitaka Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji kuandaa miradi itakayouimarisha Mfuko wa Uwezeshaji Kiuchumi ili uweze kujitegemea na kuwa endelevu.
Akizungumza kwa niaba ya Stanbic Bank Tanzania, ambayo ni mdhamini mkuu wa Tamasha la Tatu la Fahari ya Zanzibar, Mkuu wa Idara ya Biashara wa Benki hiyo, Fredrick Max, amesema Stanbic itaendelea kushirikiana na ZEEA katika kuwawezesha wafanyabiashara na wajasiriamali kukuza mitaji yao na kufikia malengo waliyojiwekea.
Max amesema wajasiriamali wanapowezeshwa kwa mitaji, kujengewa uwezo na kupatiwa vitendea kazi, huongeza thamani ya biashara zao na kuwawezesha kufikia masoko ya ndani na nje ya nchi.
Aidha amesema ushirikiano huo unalenga pia kuwafikia wafanyabiashara wadogo na wa kati kutoka Unguja na Pemba, kwa kuwapatia fursa zaidi za kifedha na kibiashara.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ZEEA, Juma Burhan Mohammed, amesema tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo mwaka 2022 hadi Agosti 2026, ZEEA imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 55.6 kwa wananchi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania – TANTRADE, Ephraim Balozi Mafuru, amesema jukumu la taasisi hiyo ni kuendeleza biashara nchini na kuongeza fursa kwa wazalishaji na wafanyabiashara.
Mafuru amesema mchango wa sekta ya biashara katika uchumi wa Tanzania ni mkubwa, akieleza kuwa bidhaa za Tanzania zilizouzwa nje ya nchi mwaka uliopita zilifikia thamani ya shilingi trilioni 26.7, kutoka shilingi trilioni 23.1, ikiwa ni ukuaji wa asilimia 15.6.
Mafuru ameahidi kuwa TANTRADE itaendelea kushirikiana na wadau kuhamasisha uzalishaji na matumizi ya vifungashio vyenye utambulisho wa Tanzania, ili bidhaa zinapouzwa nje ya nchi zitambulike kuwa ni bidhaa za Tanzania.
Naye Mkurugenzi wa kampuni ya D.light Tanzania, Mosses Cliff, ambayo inazalisha bidhaa za nishati mbadala za jua, ameishukuru Serikali na waandaaji wa Tamasha la Fahari ya Zanzibar kwa kutoa nafasi kwa kampuni na taasisi mbalimbali kushiriki maonyesho hayo.
Amesema kupitia maonyesho hayo, wananchi wanaweza kuona na kuelewa namna bidhaa za nishati mbadala zinavyoweza kuchangia maendeleo ya Zanzibar, kuongeza upatikanaji wa nishati na kuboresha maisha ya wananchi.
Tamasha la Fahari ya Zanzibar 2026 limewakutanisha wadau mbalimbali kutoka serikalini, sekta binafsi, taasisi za fedha, wajasiriamali na wazalishaji kwa lengo la kuonesha bidhaa, huduma, bunifu na fursa mbalimbali zinazopatikana Zanzibar.

Katika ufunguzi wa tamasha hilo Benki ya Stanbic Tanzania na Taasisi ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar – ZEEA, zimesaini Hati ya Makubaliano ya miaka mitano yenye lengo la kuimarisha ujasiriamali, upatikanaji wa huduma za kifedha na kukuza biashara endelevu Zanzibar.