Zenj FM
Zenj FM
31 May 2026, 14:54

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema Serikali kupitia ZIPA imekamilisha maandalizi ya kuwapokea wawekezaji wa kimataifa watakaoshiriki katika Zanzibar Investment Summit 2026.
Mary Julius.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Zanzibar Investment Promotion Authority (ZIPA) imekamilisha maandalizi ya kuwapokea wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali duniani watakaoshiriki katika mkutano mkubwa wa uwekezaji wa Zanzibar Investment Summit 2026 (ZIS 2026) unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 3 hadi 5 Juni 2026.
Akizungumza katika hafla ya ZIPA Walkathon 2026 iliyofanyika katika AFCON Fumba Grounds, Wilaya ya Magharibi “B” Unguja, Makamu wa Pili wa Rais Hemed amesema mkutano huo utawakutanisha wawekezaji wakubwa, taasisi za kifedha, wadau wa maendeleo, viongozi wa serikali pamoja na sekta binafsi kwa lengo la kujadili mustakabali wa uchumi wa Zanzibar na kuimarisha ushirikiano wa maendeleo.
Amesema Zanzibar inaendelea kujijengea nafasi ya kimataifa kama kitovu cha uwekezaji katika sekta za utalii, miundombinu, uchumi wa buluu, teknolojia na huduma za kijamii.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na wananchi katika kufanikisha maendeleo endelevu na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.
Makamu wa Pili wa Rais pia amewahimiza wananchi kuendelea kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuwa na jamii yenye afya bora na uwezo mkubwa wa kushiriki katika shughuli za uzalishaji na maendeleo ya kiuchumi.
Kwa upande wake,Waziri wa Kazi na Uwekezaji Sharif Ali Sharif amesema ZIPA Walkathon 2026 ni sehemu ya maandalizi ya mkutano wa uwekezaji wa ZIS 2026 na juhudi za kuhakikisha Zanzibar inawapokea wageni na wawekezaji katika mazingira bora.
Waziri Sharif amesema mafanikio makubwa ya maendeleo yanayoonekana Zanzibar kwa sasa yanatokana na sera na juhudi za kuvutia uwekezaji zinazoongozwa na Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Aidha Amehimiza wananchi kuendelea kushirikiana na serikali katika kuendeleza uchumi na ustawi wa jamii.
Akizungumza Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Masoud Ali Mohamed , amesema kufanyika kwa mkutano wa Zanzibar Investment Summit 2026 kutafungua fursa mbalimbali za uwekezaji zitakazoimarisha sekta ya uchumi wa buluu nchini.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ZIPA, Saleh Saad Mohamed, amesema ZIPA Walkathon 2026 imelenga kutangaza eneo la Fumba pamoja na kuonesha mafanikio ya maendeleo yanayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Nane.
Aidha Ameongeza kuwa mamlaka hiyo imekamilisha maandalizi yote muhimu ya kuwapokea wawekezaji na kuitangaza Zanzibar katika jukwaa la kimataifa la uwekezaji la Zanzibar Investment Summit 2026.