Zenj FM

Chanjo Zanzibar, asilimia 92 yafikiwa, bilioni 1.6 zatumika kila mwaka

28 May 2026, 16:20

Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya kutoka Wizara ya Afya Zanzibar, Dk. Slim Salim Slim

Wizara ya Afya Zanzibar imesema itaendelea kushirikiana na vyombo vya habari kutoa elimu ya chanjo kwa jamii ili kuhakikisha wananchi wote hususan watoto wanapatiwa chanjo kwa wakati. Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya, Dk. Slim Salim Slim, amesema Serikali hutumia zaidi ya shilingi bilioni 1.6 kila mwaka kwa ajili ya ununuzi wa chanjo mbalimbali za kujikinga na maradhi hatari. Amesema Zanzibar tayari imefikia asilimia 92 ya watoto waliochanjwa huku jitihada zikiendelea kuwafikia asilimia nane iliyobaki.

Na Mary Julius

Wizara ya Afya Zanzibar imesema itaendelea kushirikiana na vyombo vya habari katika kutoa elimu ya chanjo kwa jamii, kwa lengo la kuhakikisha Zanzibar inafikia asilimia 100 ya wananchi waliopata chanjo hususan watoto.

Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya kutoka Wizara ya Afya Zanzibar, Dk. Slim Salim Slim, ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa waandishi wa habari yaliyofanyika katika ukumbi wa Skuli ya Tumekuja.

Dk. Slim amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya uwekezaji mkubwa katika utoaji wa chanjo mbalimbali kwa watoto wachanga na wananchi kwa ujumla ili kuwakinga dhidi ya maradhi hatari ikiwemo pepopunda, surua na saratani ya shingo ya kizazi

Amesema Serikali hutumia zaidi ya shilingi bilioni 1.6 kila mwaka kwa ajili ya ununuzi wa chanjo, hatua inayolenga kuhakikisha wananchi wanakuwa salama kiafya wakati wote.

Aidha, amesema Zanzibar tayari imefikia asilimia 92 ya watoto waliochanjwa, huku akisisitiza kuwa bado jitihada zinahitajika kufikia asilimia nane iliyobaki ili kuhakikisha kila mtoto anapata chanjo kwa wakati..

Ametoa wito kwa wananchi kuondokana na dhana potofu kuhusu chanjo na badala yake kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha watoto wanapatiwa chanjo zote muhimu.

Sauti ya Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya kutoka Wizara ya Afya Zanzibar, Dk. Slim Salim Slim.

Kwa upande wake, Meneja wa Mpango wa Taifa wa Chanjo, Abdulhamid Ameir Saleh, amesema ushirikiano kati ya mpango wa chanjo na waandishi wa habari umekuwa muhimu katika kufikisha elimu kwa jamii.

Sauti ya Meneja wa Mpango wa Taifa wa Chanjo, Abdulhamid Ameir Saleh,

Kwa upande wake, Afisa Mratibu wa Ufuatiliaji wa Maradhi Yanayokingwa na Chanjo Zanzibar, Ibrahim Juma Ibrahim, amewasisitiza wazazi na jamii kuhakikisha kila mtoto anapatiwa chanjo kwa wakati ili kumuwezesha kuwa na afya bora na kutimiza ndoto zake za maisha.

Sauti ya Afisa Mratibu wa Ufuatiliaji wa Maradhi Yanayokingwa na Chanjo Zanzibar, Ibrahim Juma Ibrahim,