Zenj FM
Zenj FM
20 July 2026, 23:02

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja linamshikilia mtu mmoja kwa tuhuma za kumuua mwanaume mwenye umri wa miaka 40 katika eneo la Tunguu Ipa, Wilaya ya Kati, kufuatia ugomvi unaodaiwa kusababishwa na kutokuelewana. Polisi wamewahimiza wananchi kutatua migogoro kwa njia ya mazungumzo na kufuata sheria ili kuepusha vitendo vya vurugu vinavyoweza kusababisha kupoteza
Na Mary Julius.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja linamshikilia mtu mmoja kwa tuhuma za mauaji yaliyotokea katika eneo la Tunguu Ipa, Wilaya ya Kati.
Akizungumza na Zenj Fm, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Daniel Emanuel Shillah, amesema tukio hilo lilitokea Julai 18 majira ya saa 5:30 usiku.
Amesema mtuhumiwa, Masanja Juma Ezekiel, mwenye umri wa miaka 25, mkazi wa Tunguu Ipa na mwenyeji wa Mwanza, anadaiwa kumuua Khamis Omari Salum, mwenye umri wa miaka 40, mkazi wa Tunguu Ipa na mwenyeji wa Morogoro, kwa kumchoma kisu sehemu za shingoni na kichwani.
Kwa mujibu wa Kamanda Shillah, chanzo cha tukio hilo kinadaiwa kuwa ni ugomvi uliotokana na kutokuelewana baada ya marehemu kung’oa chaga za kitanda na kuzitupa nje, jambo lililosababisha mabishano yaliyogeuka kuwa vurugu.
Ameeleza kuwa wakati wa ugomvi huo, mtuhumiwa anadaiwa kutumia kisu kumshambulia marehemu, na kusababisha majeraha makubwa kichwani na shingoni. Marehemu alifariki dunia kutokana na kuvuja damu nyingi.
Kamanda Shillah amesema mtuhumiwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi, na hatua za kisheria zitachukuliwa baada ya uchunguzi kukamilika.
Aidha, JKamnada Shillah ametoa wito kwa wananchi kutatua migogoro kwa njia ya mazungumzo na kufuata taratibu za kisheria badala ya kutumia vurugu au silaha, ili kuepusha madhara, majeraha na kupoteza maisha.