Zenj FM
Zenj FM
14 June 2026, 13:36

Walimu na wazazi wametakiwa kushirikiana kuhakikisha watoto wote wa kike wenye umri wa miaka tisa wanapata chanjo ya HPV kwa ajili ya kujikinga na saratani ya shingo ya kizazi. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inalenga kuwachanja watoto 28,498 wanaostahili huduma hiyo mwaka 2026 katika Unguja na Pemba.
Na Mary Julius.
Walimu na wazazi wametakiwa kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha watoto wote wa kike wenye umri wa miaka tisa wanapata chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi, Chanjo ya HPV (Human Papillomavirus Vaccine). ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwalinda dhidi ya ugonjwa huo hatari.
Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar inalenga kuwafikia watoto 28,498 wa Unguja na Pemba wanaostahili kupatiwa chanjo hiyo kwa mwaka 2026.
Akizungumza na ZENJ FM katika kipindi cha Mwangaza wa Habari, Mratibu wa Shughuli za Chanjo Wilaya ya Magharibi B, Zuwena Salimu Abdullah, amesema wilaya hiyo imefanikiwa kuwafikia asilimia 77 ya watoto waliolengwa kuchanjwa, ambapo kati ya watoto 5,252 wanaostahili chanjo hiyo, wengi wao tayari wamepatiwa huduma hiyo.
Zuwena amesema miongoni mwa changamoto zinazokwamisha juhudi za utoaji wa chanjo hiyo ni baadhi ya skuli binafsi kutotoa ushirikiano wa kutosha, jambo linaloathiri uwezo wa kuwafikia watoto wote wanaostahili kupatiwa chanjo.
Naye Muuguzi Mkunga na Mhamasishaji wa Mpango wa Chanjo kwa Unguja na Pemba, Ruzuna Abdulrahimu Mohamed, amewataka wazazi kujitokeza na kutoa ushirikiano ili kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo hiyo inayolenga kuzuia saratani ya shingo ya kizazi na kulinda afya ya kizazi kijacho.
Aidha, amewashauri wanawake kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara, angalau mara mbili kwa mwaka, ili kubaini mapema magonjwa mbalimbali ikiwemo saratani ya shingo ya kizazi, ambayo amesema mara nyingi hujificha bila dalili za awali na inaweza kusababisha madhara makubwa endapo haitagundulika mapema.
Kwa mujibu wa takwimu za mpango wa chanjo, jumla ya watoto 28,498 wenye umri wa miaka tisa wanatarajiwa kuchanjwa Zanzibar kwa mwaka 2026. Kati yao, watoto 20,342 wanatoka Unguja na 8,156 wanatoka Pemba.