Zenj FM
Zenj FM
1 June 2026, 16:48

Wafanyabiashara wa Shehia za Jumbi na Tunguu wamehimizwa kutunza usafi wa mazingira katika maeneo yao ya biashara ili kuzuia magonjwa yanayosababishwa na uchafu. Wito huo umetolewa na Mkuu wa Divisheni ya Mazingira na Mipango Miji wa Baraza la Manispaa Kati, Amour Badali Amour, wakati wa mafunzo ya usafi yaliyofanyika Jumbi.
Na Hakika Mwinyi.
Wafanyabiashara wa Shehia za Jumbi na Tunguu wametakiwa kutambua na kutekeleza wajibu wao wa kutunza na kuhifadhi mazingira katika maeneo yao ya biashara ili kujikinga na kuzuia kuenea kwa maradhi yanayotokana na uchafuzi wa mazingira.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Divisheni ya Mazingira na Mipango Miji wa Baraza la Manispaa Kati, Amour Badali Amour, wakati wa kutoa elimu ya usafi na utunzaji wa mazingira kwa wafanyabiashara hao katika Skuli ya Msingi Jumbi, Wilaya ya Kati.
Amesema wafanyabiashara wana nafasi kubwa katika kuhakikisha mazingira ya maeneo yao ya biashara yanakuwa safi wakati wote, akisisitiza kuwa mapambano dhidi ya uchafu yanahitaji ushiriki wa kila mmoja kwa kuzingatia taratibu za usafi na utunzaji wa mazingira.
Kwa upande wake, Sheha wa Shehia ya Jumbi, Muhidini Haji Machano, amesema suala la usafi si jukumu la mtu mmoja au taasisi moja pekee, bali linahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Baraza la Manispaa na wananchi ili kufanikisha mazingira safi na salama kwa wote.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Usafi, Haji Mohammed Iddi, ameiomba Manispaa Kati kuimarisha huduma za ukusanyaji taka kwa kuzichukua kwa wakati, huku akiwataka wafanyabiashara kutumia maeneo rasmi yaliyotengwa kwa ajili ya kutupa taka.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wenzake, Asia Habibu amesema wanakabiliwa na changamoto ya kuchelewa kuchukuliwa kwa taka katika maeneo yao ya biashara, jambo ambalo huathiri usafi wa mazingira. Ameiomba Manispaa Kati kutafuta suluhisho la kudumu kwa changamoto hiyo.
Zaidi ya wafanyabiashara 50 kutoka Shehia za Jumbi na Tunguu wamepatiwa elimu, maelekezo na ufafanuzi kuhusu umuhimu wa usafi na utunzaji wa mazingira, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupambana na uchafu na kuimarisha afya za wananchi katika maeneo ya biashara.