Zenj FM

Ulinzi shirikishi wadumisha usalama Kusini Unguja

1 June 2026, 15:50

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis akiwa katika hafla ya kukabidhi vyeti vya pongezi na zawadi kwa askari waliofanya vizuri katika maeneo yao ya kazi.

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja amelipongeza Jeshi la Polisi kwa mafanikio makubwa ya kupunguza matukio ya uhalifu na kuimarisha usalama katika jamii. Akizungumza katika hafla ya utoaji wa zawadi kwa askari waliofanya vizuri, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya polisi na wananchi.

Na Mary Julius

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na Usalama ya Mkoa, amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi kubwa ya kupunguza matukio ya kihalifu katika jamii, akisema anajivunia utendaji wa jeshi hilo katika kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi vyeti vya pongezi na zawadi kwa askari waliofanya vizuri katika maeneo yao ya kazi, iliyofanyika Machui, Mkuu huyo wa Mkoa Hamida  amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kupunguza uhalifu, bado kuna umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya polisi na wananchi.

Amesema hatua hiyo itasaidia kujenga mahusiano mazuri, kuondoa pengo lililopo kati ya pande hizo mbili na kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa misingi ya utu, uadilifu na weledi.

Aidha, amewataka askari wanaopangiwa maeneo mbalimbali kuhakikisha wanaifahamu vizuri jamii wanayoihudumia ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi, na amesisitiza kuwa askari wa shehia wana nafasi muhimu katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika ngazi ya msingi.

Sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis.

Kuhusu usalama barabarani, Mkuu wa Mkoa Hamida  amewataka askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani kuongeza umakini katika kudhibiti ajali zinazotokana na uzembe wa baadhi ya madereva, hususan wa magari makubwa.

Sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis .

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Daniel Emmanuel Shillah, amesema utoaji wa vyeti vya pongezi na zawadi ni chachu kwa askari na watumishi wa jeshi hilo, kwani unawapa hamasa ya kuongeza bidii katika kazi na kuwahamasisha wengine kujituma zaidi.

Amesema dhamira kuu ya Jeshi la Polisi ni kutoa huduma bora kwa wananchi ili waweze kutekeleza shughuli zao za kijamii na kiuchumi katika mazingira salama na yenye utulivu.

Aidha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja amesema Jeshi la Polisi litaendelea kuweka nguvu katika kuimarisha ushirikiano na jamii ili wananchi waweze kulielewa vyema jeshi hilo na kutambua kuwa lipo karibu nao wakati wote katika kuhakikisha amani na usalama vinadumishwa.

Sauti ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Daniel Emmanuel Shillah.

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis akimkabidhi zawadi Sajenti Hassan M Ali ambaye ni anatokea katika Kitengo cha Uchunguzi wa Kisanjansi  cha Mkoa wa Kusini Unguja .

Kwa upande wao, baadhi ya askari waliotunukiwa vyeti vya pongezi na zawadi kwa utendaji bora Sajenti Abdllah Hassan  Kitengo cha Traffic na Sajenti Hassan M Ali ambaye anatokea katika Kitengo cha Uchunguzi wa Kisanjansi  cha Mkoa wa Kusini Unguja wamesema wataendelea kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na weledi ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.

Aidha Wamesema kutambuliwa na kupewa zawadi hizo kumekuwa chachu na hamasa ya kuongeza juhudi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, huku wakiahidi kuendelea kushirikiana na wananchi katika kulinda usalama wa jamii.

Sauti ya waliotunukiwa zawadi.

Katika hafla hiyo, zawadi na vyeti vya pongezi vimetolewa kwa askari binafsi  8 waliofanya vizuri katika maeneo tofauti ya utendaji.