Zenj FM

Jamii yahimizwa kushiriki malezi na ustawi wa watoto yatima

30 June 2026, 22:16

.Diwani wa Kuteuliwa wa Wilaya ya Kati, Amina Andrew Clement akiwa na watoto yatima katika Kituo cha Kulelea Yatima MAFTUH FOUNDATION kilichopo Kibele pamoja na watoto yatima wa Shehia ya Bambi, Wilaya ya Kati Unguja.

Diwani wa Kuteuliwa wa Wilaya ya Kati, Mhe. Amina Andrew Clement, ametoa wito kwa viongozi na wadau kuendelea kutembelea na kuwasaidia watoto yatima ili kuwapa faraja na kuwafanya wajisikie kuwa sehemu ya jamii. Katika ziara yake ya Kituo cha Maftuh Foundation Kibele na Shehia ya Bambi, watoto yatima 108 walinufaika na msaada wa chakula pamoja na mahitaji muhimu.

Na Hakika Mwinyi.

Viongozi na wadau mbalimbali wametakiwa kujitokeza kwa wingi kutembelea vituo vya kulelea watoto yatima ili kuwafariji na kuwafanya wajisikie kuwa sehemu ya jamii kama watoto wengine.

Rai hiyo imetolewa na Diwani wa Kuteuliwa wa Wilaya ya Kati, Amina Andrew Clement, wakati alipotembelea Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Maftuh Foundation kilichopo Kibele pamoja na watoto kutoka Shehia ya Bambi, Wilaya ya Kati Unguja.

Amesema ziara hiyo ni sehemu ya kutekeleza majukumu ya kijamii ya viongozi, akibainisha kuwa madiwani wana wajibu wa kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto mbalimbali za jamii.

Ameeleza kuwa uamuzi wake wa kuwatembelea watoto hao, kuwajulia hali na kuwapatia sadaka unalenga kuwapa faraja na kuimarisha ukaribu kati ya viongozi na watoto wanaoishi kwenye mazingira hayo.

Sauti ya Diwani wa Kuteuliwa wa Wilaya ya Kati, Amina Andrew Clemen

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Maftuh Foundation, Fatma Ali Maftuh, amesema malezi ya watoto yatima si jukumu la vituo pekee bali ni wajibu wa jamii nzima.

Amesema watoto hao wana mahitaji mbalimbali yanayohitaji ushirikiano wa wadau na wahisani ili waweze kuishi katika mazingira yanayowafanya wajisikie sawa na watoto wengine.

Sauti ya Mkurugenzi wa Kituo cha Maftuh Foundation, Fatma Ali Maftuh,

Naye, Fauzia Mussa Juma, akizungumza kwa niaba ya watoto wenzake, amemshukuru Diwani Amina Andrew Clement kwa kuwafikia, kuwafariji na kuwapatia sadaka. Pia ametoa wito kwa wahisani, wadau na wananchi wenye uwezo kuendelea kutembelea kituo hicho na kutoa misaada mbalimbali kwa ajili ya watoto hao.

Sauti ya Fauzia Mussa Juma,

Katika ziara hiyo, jumla ya watoto yatima 108 walinufaika, ambapo 52 ni kutoka Kituo cha Maftuh Foundation Kibele na 56 kutoka Shehia ya Bambi.

Zaidi ya shilingi milioni 2.146 zilitumika kununua sadaka mbalimbali, zikiwemo mifuko ya mchele yenye uzito wa kilo 200, ng’ombe mmoja, paketi sita za sabuni ya unga, galoni nne za sabuni ya maji, dustbin mbili ndogo pamoja na ndoo mbili za kunawia zenye mfumo wa maji yanayotiririka.

.