Zenj FM
Zenj FM
7 June 2026, 23:33

Skuli ya Assalam International imepongezwa kwa juhudi zake za kuhifadhi mazingira na kuhamasisha uhifadhi wa bahari wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani. Viongozi na wananchi wamezitaka taasisi nyingine kuiga mfano huo ili kulinda mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Na Mary Julius.
Afisa wa Watu Wenye Ulemavu Wilaya ya Kusini Unguja, Ussi Khamis Ussi, akizungumza kwa niaba ya Afisa Mazingira wa Wilaya hiyo, amezitaka skuli na taasisi mbalimbali kuiga mfano wa Skuli ya Assalam International katika juhudi za kulinda na kuhifadhi mazingira.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyoandaliwa na Skuli ya Assalam International sambamba na kampeni ya kuhamasisha uhifadhi wa bahari, Ussi amesema hatua zinazochukuliwa na skuli hiyo zinaunga mkono juhudi za Serikali katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha mazingira yanabaki salama kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Naye Afisa anayeshughulikia Skuli za Maandalizi ya Elimu ya Msingi, Sekondari na Skuli Binafsi Wilaya ya Kusini Unguja, Mahfoudh Said Omar, amesema jamii ina wajibu wa kutunza mazingira ili kujikinga na maradhi yanayosababishwa na uchafuzi wa mazingira.
Amesema Skuli ya Assalam International imekuwa mdau muhimu katika kueneza elimu ya mazingira kwa wanafunzi na jamii, huku akisisitiza kuwa uhifadhi wa mazingira ni jukumu la kila mwananchi.

Kwa upande wake, Mwalimu wa skuli hiyo, Huzaima Abdalla Mzee, amesema Assalam International inatekeleza programu ya kimataifa inayohamasisha shule kushiriki katika uhifadhi wa mazingira na maendeleo endelevu kupitia ushirikiano wa wanafunzi, walimu na jamii.
Aidha Amefafanua kuwa programu hiyo inawajengea wanafunzi uelewa kuhusu usimamizi wa taka, upandaji miti, matumizi bora ya maji na nishati pamoja na mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Skuli ya Assalam International, Said Hamad, amesema elimu ya mazingira kwa vijana ni msingi muhimu wa kuandaa kizazi kitakachokuwa mstari wa mbele katika kulinda rasilimali za asili nchini.
Nao wazazi walioshiriki katika maadhimisho hayo wameahidi kuendelea kuhamasisha usafi wa mazingira katika maeneo yao na kuwashauri wananchi kuepuka kutupa taka za plastiki baharini ili kulinda viumbe hai wa baharini na kuhifadhi rasilimali za bahari kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.