Zenj FM

Rais Mwinyi aongeza kima cha chini cha mshahara hadi Sh. 500,000 Zanzibar

1 May 2026, 2:58 pm

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi) yaliyofanyika Kizimbani.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Hussein Ali Mwinyi ametangaza kuongeza kima cha chini cha mshahara kutoka shilingi 300,000 hadi 500,000 kwa mwezi katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi tarehe 01 Mei 2026.
Amesema mshahara huo mpya utaanza kutekelezwa Januari 2027 baada ya kuzingatia hali ya uchumi na gharama za maisha ili kuongeza motisha kwa wafanyakazi.

Na Mary Julius.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametangaza kuongeza kima cha chini cha mshahara kutoka shilingi 300,000 hadi shilingi 500,000 kwa mwezi.

Ametoa tangazo hilo , wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi) yaliyofanyika Kizimbani. Amesema mshahara huo mpya utaanza kutumika rasmi Januari 2027, ukiwa na lengo la kuboresha maisha ya wafanyakazi pamoja na kuongeza motisha kazini.

Rais Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya kazi, kuhakikisha stahiki za wafanyakazi zinalipwa kwa wakati, na kushirikiana kwa karibu na vyama vya wafanyakazi katika kutatua changamoto mbalimbali.

Aidha, Rais Dkt Mwinyi ametangaza ajira mpya 7,500 kwa mwaka wa fedha 2026/2027, huku akiwataka wafanyakazi kufanya kazi kwa bidii, nidhamu na uzalendo ili kuchochea maendeleo ya Zanzibar.

Sauti ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi,

Kwa upande wake, Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Sharif Ali Sharif, amesema katika mwaka uliopita changamoto 29 ziliwasilishwa, ambapo 24 kati yake zilitatuliwa, na zilizobaki tayari zimepatiwa maelekezo ya Rais kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi.

Akizungumzia ongezeko la mshahara kwa zaidi ya asilimia 70 amesema ongezeko hilo linapaswa kuwa chachu kwa wafanyakazi kuongeza juhudi kazini.

Sauti ya Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Sharif Ali Sharif.

Akisoma risala ya wafanyakazi, Katibu Mkuu wa ZATUC, Khamis Mwinyi Mohammed, ameishukuru Serikali kwa kutekeleza maombi 11 kati ya 14 yaliyowasilishwa awali, yakiwemo marekebisho ya sheria, uboreshaji wa haki za wafanyakazi, na ushiriki wao katika maamuzi ya kiutendaji.

Ameomba maboresho zaidi, hususan katika sekta binafsi, ikiwemo mishahara, posho, mazingira ya kazi vijijini, pamoja na kuondolewa kwa kanuni zinazokwenda kinyume na sheria. Pia amesisitiza umuhimu wa kuboresha mifumo ya mawasiliano ili kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wafanyakazi.

Sauti ya Khamis Mwinyi Mohammed.