Zenj FM

Vijana watakiwa kulinda maadili na heshima ya Taifa

14 June 2026, 15:31

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar, Sultan Said Suleiman Akizungumza katika mahafali ya 11 ya kidato cha sita yaliyofanyika katika Skuli ya Hamamni.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar, Sultan Said Suleiman, amewahimiza wahitimu wa kidato cha sita kutokata tamaa na kuzingatia nidhamu, bidii na kujiamini ili kufikia mafanikio. Amesema vijana wanapaswa kutumia maarifa na vipaji vyao kujiajiri, kuajiri wengine.

Na Mary Julius

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar, Sultan Said Suleiman, amewataka wanafunzi wahitimu wa kidato cha sita kutokata tamaa katika safari yao ya maisha, akisisitiza kuwa mafanikio makubwa hujengwa kwa uvumilivu, nidhamu, bidii na kujiamini.

Akizungumza katika mahafali ya 11 ya kidato cha sita yaliyofanyika katika Skuli ya Hamamni, amesema dunia ya sasa inahitaji vijana wabunifu wenye ujasiri wa kutumia maarifa na vipaji vyao kujiajiri na kuajiri wengine huku wakichangia maendeleo ya jamii.

Aidha amesema taifa linawahitaji vijana hao kuwa viongozi wa baadaye, hivyo ni muhimu kuendelea kusoma kwa bidii, kulinda heshima ya nchi yao na kushikamana na maadili mema.

Sauti ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar, Sultan Said Suleiman.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Hamamni, Khamis Hamad Khamisi,  amepongeza juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi kwa  kuimarisha sekta ya elimu na kuhakikisha vifaa vya kufundishia vinapatikana kwa wakati pamoja na kuwepo kwa walimu wa kutosha mashuleni.

Aidha, amewataka wazazi na wanafunzi kuachana na tuition za mitaani, akieleza kuwa mtaala mpya unahitaji walimu waliopata mafunzo rasmi ya kuufundisha, ambao tayari wanapatikana mashuleni.

Sauti ya Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Hamamni, Khamis Hamad Khamisi,

Akisoma risala ya wahitimu, mwanafunzi Mudrik Mohammed amesema jumla ya wanafunzi 330 walihitimu, wakiwemo wavulana 147, huku wanafunzi watatu wakishindwa kufanya mitihani yao.

Ameishukuru Wizara ya Elimu kwa kuwapatia walimu waliowafundisha kwa ufanisi na kuahidi kuwa wahitimu watafanyia kazi mafunzo yote waliyopewa.

Aidha Wahitimu hao pia wameeleza changamoto zinazowakabili, ikiwemo uhaba wa vitabu katika maktaba pamoja na kutokuwepo kwa photocopy machine na printer, na kuiomba serikali pamoja na wadau wa elimu kulifanyia kazi suala hilo kwa manufaa ya wanafunzi wanaoendelea na masomo.

Sauti ya Mudrik Mohammed.

Kwa upande wao, wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo yao wamesema nidhamu imekuwa msingi mkubwa wa mafanikio yao, wakisisitiza umuhimu wa kuheshimu walimu, wazazi na jamii inayowazunguka.

Wamewahimiza wanafunzi wanaobaki kuongeza juhudi, bidii na kujituma katika kila kazi wanayopewa ili kufikia malengo yao.

Aidha wamewataka wanafunzi wa kike kutokata tamaa na kuendelea kupambana ili kufikia ndoto zao za elimu na maendeleo ya baadaye.

Sauti ya wanafunzi.