Zenj FM

Maji machafu yagharimu nyumba tano Magogoni zapigwa faini ya shilingi 50,000

15 June 2026, 14:05

Mtaro wa maji machafu ulio kutana na bomba la maji ya safi Magogoni.

Nyumba tano katika eneo la Magogoni, Wilaya ya Magharibi “B” Unguja, zimepigwa faini ya shilingi 50,000 kila moja kwa kosa la kutiririsha maji machafu katika maeneo ya wazi na kuchafua mazingira. Hatua hiyo imechukuliwa na Manispaa ya Magharibi “B” kupitia operesheni maalumu ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira na kulinda afya za wananchi.

Na Mariamu Seif.

Manispaa ya Magharibi “B” imetoza faini ya shilingi elfu 50 kwa nyumba tano zilizopo katika eneo la Magogoni, Wilaya ya Magharibi “B” Unguja, kwa kosa la uchafuzi wa mazingira kupitia utiririshaji wa maji machafu katika maeneo ya wazi.

Hatua hiyo imechukuliwa katika operesheni maalumu iliyoongozwa na Afisa Habari, Uhusiano na Elimu wa Manispaa hiyo, Khamis Said Saleh, iliyolenga kubaini na kudhibiti vitendo vya uchafuzi wa mazingira katika eneo la Magogoni.

Amesema kuwa nyumba hizo zimekutwa zikiweka mitaro ya maji machafu na mashimo ya makaroni katika maeneo yasiyo rasmi, hali inayoweza kuhatarisha afya za wananchi wengine.

 Khamis amesema Manispaa itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya uchafuzi wa mazingira ili kuzuia vitendo hivyo kujirudia.

Aidha, amewataka wananchi kuchimba mashimo maalumu ya kuhifadhi maji machafu na kuwa walinzi wa mazingira katika maeneo yao.

Sauti ya Afisa Habari, Uhusiano na Elimu wa Manispaa hiyo, Khamis Said Saleh.