Zenj FM
Zenj FM
28 June 2026, 03:39

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeahidi kuimarisha ubora wa huduma za afya kwa kuhakikisha uwekezaji uliofanywa katika sekta hiyo unawanufaisha wananchi moja kwa moja. Wadau wa afya wameeleza kuwa ushirikiano, matumizi ya takwimu na ufuatiliaji wa viwango vya huduma ni nguzo muhimu za kufikia huduma bora ifikapo mwaka 2030.
Na Mary Julius
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeeleza kuwa itaendelea kuimarisha ubora wa huduma za afya kwa kuhakikisha uwekezaji uliofanywa katika miundombinu, vifaa tiba na teknolojia unaleta matokeo chanya kwa wananchi.
Akizungumza katika Mkutano wa Wadau wa Afya kuhusu kuendeleza utoaji wa huduma bora kwa kipindi cha mwaka 2026 hadi 2030, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar Dkt Mngereza Mzee Miraji, amesema viongozi wote wa sekta ya afya wanapaswa kuwajibika kuhakikisha kila hospitali, kituo cha afya na zahanati vinatoa huduma zinazokidhi matarajio ya wananchi.
Amesema Serikali imeweka vipaumbele vitano muhimu kuelekea mwaka 2030, ambavyo ni kuboresha ubora wa huduma na usalama wa wagonjwa, kuimarisha mfumo wa rufaa, kuendeleza uongozi na uwajibikaji, kutumia mifumo ya kidijitali na takwimu katika maamuzi, pamoja na kuimarisha rasilimali watu na utamaduni wa huduma kwa mteja.
Katibu Mkuu Dkt Mngereza, amewataka Wakurugenzi, Wakuu wa Hospitali, Maafisa wa Afya wa Wilaya na viongozi wote wa sekta hiyo kuandaa mipango ya utekelezaji yenye malengo yanayopimika, viashiria vya mafanikio na mfumo wa ufuatiliaji wa kila robo mwaka.
Kwa upande wake, Msimamizi Mkuu wa Miradi wa PharmAccess Zanzibar Faiza Bwanakheri Abassi amesema taasisi hiyo imeendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Afya Zanzibar katika kuandaa miongozo ya kitaalamu itakayowezesha kufuatilia na kupima ubora wa huduma zinazotolewa katika hospitali na vituo vya afya.
Amesema lengo kuu la miongozo hiyo ni kuhakikisha kila kituo cha afya kinafanya kazi kwa kuzingatia viwango vya ubora, huku changamoto zinazobainika zikitafutiwa ufumbuzi kwa wakati ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mratibu wa mfumo wa ZHSF Mother, Mayasa Suleiman Omar, amesema mfumo huo umefanikiwa kuwafikia wajawazito 2,861 katika wilaya 2 kwa muda wa miaka miliwi ikiwa na lengo la kuwafikia wakina mamaelfu tano.
Hata hivyo, tathmini imeonyesha kuwa asilimia 70.9 ya wajawazito waliofikiwa walikuwa na upungufu wa damu, jambo linaloonyesha umuhimu wa kuendelea kuimarisha huduma za lishe na ufuatiliaji wa wajawazito.
Mayasa amesema changamoto zilizobainika ni pamoja na idadi ndogo ya wajawazito wanaokamilisha mahudhurio yote nane ya kliniki na ufuatiliaji hafifu baada ya kujifungua.
Aidha Amewataka Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kuhakikisha kila mama anayejifungua anafuatiliwa ndani ya siku saba za kwanza baada ya kujifungua.
Kwa upande wake, Dkt. Sumaiya Musa amesema tathmini ya udhibiti wa maambukizi hospitalini imeonyesha mafanikio katika upatikanaji wa maji, maeneo ya kunawia mikono, vitakasa mikono na kuboreshwa kwa mazingira katika baadhi ya vituo vya afya.
Aidha , amesema bado kuna changamoto katika usimamizi wa programu za udhibiti wa maambukizi, usafi wa mazingira, uchakataji wa vifaa tiba na utunzaji wa taka za hospitali.