Zenj FM

Zaidi ya wananchi 420 wanufaika na kambi ya afya jimbo la Amani

20 July 2026, 22:36

Mwalimu mkuu msaidizi wa skuli ya Kilimahewa Mwalimu Mohammed Mwalimu akipatiwa huduma ya kupima afya katika kambi ya Kilimahewa.

Zaidi ya wananchi 420 wamejitokeza kupima afya zao katika kambi ya huduma za afya ya siku mbili iliyoandaliwa katika Jimbo la Amani, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha uchunguzi wa mapema na kinga dhidi ya magonjwa. Viongozi wa jimbo hilo wamewahimiza wananchi kuendelea kutumia fursa za huduma za afya zinazowafikia karibu na makazi yao ili kubaini changamoto za kiafya mapema na kupata matibabu kwa wakati.

Na Mary Julius.

Zaidi ya wananchi 420 wamejitokeza kupima afya zao katika Kambi ya siku mbili ya huduma za afya iliyoandaliwa katika Jimbo la Amani, hatua iliyoonesha kuongezeka kwa uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa uchunguzi wa afya kwa ajili ya kujikinga na magonjwa.

Akizungumza katika kambi hiyo iliyodumu kwa siku mbili, Mbunge wa Jimbo la Amani, Abdull Yussuf Maalim, amesema lengo la huduma hizo ni kuwapa wananchi fursa ya kufahamu hali zao za kiafya mapema ili kujenga jamii yenye afya bora.

Mbunge Maalim amesema kwa mujibu wa ripoti ya madaktari waliotoa huduma, changamoto kubwa zilizobainika ni matatizo ya macho pamoja na saratani ya shingo ya kizazi.

Aidha mbunge Maalim ameeleza kuwa wananchi watakaobainika kuwa na changamoto mbalimbali wataunganishwa na huduma stahiki ili kuhakikisha wanapata matibabu yanayohitajika kwa wakati.

Sauti ya Mbunge wa Jimbo la Amani, Abdull Yussuf Maalim.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Jimbo la Amani, Masoud Amour Masoud, amesema viongozi wa jimbo hilo wameungana kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya, akieleza kuwa hatua hiyo inaunga mkono juhudi za Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi za kuimarisha huduma za afya nchini.

Aidha amesema kambi hiyo imewahudumia wakazi wa Jimbo la Amani, Wadi ya Kilima Hewa pamoja na shehia zote nne za jimbo hilo.

Sauti ya Mwakilishi wa Jimbo la Amani, Masoud Amour Masoud,.

Naye Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Kilima Hewa na Naibu Katibu wa Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Kisukari Zanzibar, Rukia Makungu Mgongo, amesema taasisi yao imeungana na viongozi wa Jimbo la Amani kuwafikia wananchi ambao mara nyingi hawafiki vituo vya afya, ili kuwagundua mapema wenye magonjwa yasiyoambukiza na kuwawezesha kuanza matibabu kwa wakati.

Rukia ametoa wito kwa viongozi wa majimbo mengine kuiga mfumo huo wa kupeleka huduma za afya karibu na wananchi,

Sauti ya Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Kilima Hewa na Naibu Katibu wa Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Kisukari Zanzibar, Rukia Makungu Mgongo.

Kwa upande wake, Diwani wa Kilima Hewa, Akida Juma Makame, amewahimiza wananchi kuendelea kujitokeza kila zinapoandaliwa kambi kama hizo na kuwapongeza viongozi kwa kuwasogezea huduma muhimu karibu na makazi yao.

Sauti ya Diwani wa Kilima Hewa, Akida Juma Makame

Nao baadhi ya wananchi walionufaika na huduma hizo wameelezea kuridhishwa na ubora wa huduma walizopata. Mkazi wa Shehia hiyo, Salma Musas Yusuff, amesema wananchi wamepokea kwa furaha huduma hizo kutokana na manufaa makubwa ya uchunguzi wa afya, huku akiomba ziwe endelevu ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Wananchi.