Zenj FM

Haki za Watu wenye ulemavu zapewa kipaumbele Zanzibar

18 September 2026, 14:20

Kaimu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Hamza Hassan Juma.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema utekelezaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Watu Wenye Ulemavu, CRPD, umeimarisha sera, sheria na mifumo ya utoaji huduma na ulinzi wa haki za watu wenye ulemavu, huku ukiongeza ushiriki wa asasi zao na kupata misaada ya kitaalamu na kifedha.

Na Mary Julius

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema utekelezaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Watu Wenye Ulemavu, maarufu kama CRPD, umeleta manufaa makubwa katika kuimarisha sera, sheria na mifumo ya ulinzi na uendelezaji wa haki za watu wenye ulemavu nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Hamza Hassan Juma, wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Chake Chake, Abdulwahab Said Abubakar, aliyetaka kujua namna Zanzibar ilivyonufaika na utekelezaji wa mkataba huo, pamoja na msaada wa kitaalamu na kifedha uliopatikana.

Waziri Hamza amesema changamoto na mapendekezo yaliyoibuliwa kupitia mchakato wa utekelezaji wa CRPD yamesaidia kuimarisha utekelezaji wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Na. 8 ya mwaka 2022, sambamba na kuboresha mifumo ya utoaji wa huduma na fursa kwa watu wenye ulemavu.

Amesema pia utekelezaji wa mkataba huo umeongeza ushiriki wa Asasi za Watu Wenye Ulemavu, OPDs, katika kufuatilia na kutetea haki zao, ikiwemo kuandaa na kuwasilisha taarifa mbadala, maarufu kama Shadow Reports, kwa Kamati ya Umoja wa Mataifa.

Kwa upande wa msaada, Serikali imesema Zanzibar imeendelea kupata misaada ya kitaalamu na kifedha kutoka kwa mashirika mbalimbali ya kitaifa na kimataifa, yakiwemo Zanzibar Milele Foundation, UNICEF, UNFPA na UNDP, pamoja na Asasi za Kiraia.

Kwa mujibu wa Serikali, misaada hiyo imeelekezwa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo elimu jumuishi, afya, uwezeshaji wa kiuchumi na uimarishaji wa haki za watu wenye ulemavu.

Aidha, Serikali imesema utekelezaji wa CRPD umechangia kuboresha mifumo ya ukusanyaji na matumizi ya takwimu kuhusu watu wenye ulemavu, jambo linalosaidia katika upangaji wa bajeti jumuishi, utoaji wa huduma na maandalizi ya mipango inayozingatia mahitaji yao.

Sauti ya Kaimu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Hamza Hassan Juma.

Akiuliza swali la nyongeza.Mwakilishi wa Jimbo la Paje, Jaku Hashim Ayubu, amehoji utekelezaji wa sheria inayohusu watu wenye ulemavu, akitaka kujua hatua zinazochukuliwa na Serikali kuhakikisha wakandarasi wanazingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu wakati wa ujenzi wa majengo.

Mwakilishi Jaku pia ameuliza kuhusu jumuiya iliyokuwa ikitumia jengo la ZBS Maruhubi, baada ya kuondolewa katika jengo hilo, akitaka kujua imehamishiwa wapi na hatua zilizochukuliwa dhidi ya watu wanaodaiwa kuwadhihaki watu wenye ulemavu Zanzibar.

Sauti ya Mwakilishi wa Jimbo la Paje, Jaku Hashim Ayubu.

Akijibu maswali hayo.Waziri Hamza amesema sheria ipo na kwamba Bodi ya Wakandarasi imeweka masharti yanayozingatia mahitaji maalum ya watu wenye ulemavu katika ujenzi wa majengo.

Amesema wakandarasi wanatakiwa kuzingatia mahitaji hayo wakati wa ujenzi ili kuhakikisha majengo yanakuwa rafiki na yanayoweza kutumiwa na watu wenye ulemavu.

Kuhusu jumuiya iliyokuwa ikitumia jengo la ZBS Maruhubi, Waziri amesema jengo hilo halikuwa mali ya jumuiya hiyo moja kwa moja.

Amesema Mkuu wa Wilaya wa Mjini ametoa eneo jingine lililopo Chumbuni, na kwamba Serikali inaendelea na maandalizi ya kulifanyia matengenezo jengo hilo ili liweze kutumika na jumuiya hiyo.

Sauti ya Kaimu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Hamza Hassan Juma.