Zenj FM

Zanzibar yasema ipo salama dhidi ya Ebola, yazidi kuimarisha ulinzi wa mipaka

28 May 2026, 17:22

Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya kutoka Wizara ya Afya Zanzibar, Dk. Slim Salim Slim,

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema Zanzibar bado ipo salama dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa Ebola na inaendelea kuimarisha ulinzi wa afya mipakani ili kuzuia ugonjwa huo kuingia nchini.

Na Mary Julius

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema Zanzibar bado ipo salama dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa Ebola na kwamba inaendelea kuimarisha ulinzi wa afya katika mipaka yake ili kuzuia ugonjwa huo kuingia nchini.

Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya kutoka Wizara ya Afya Zanzibar, Dk. Slim Salim Slim, wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa waandishi wa habari yaliyofanyika katika ukumbi wa Skuli ya Tumekuja.

Dk. Slim amesema baadhi ya nchi za Afrika ikiwemo Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimeendelea kukumbwa na ugonjwa huo ambao unasambaa kwa kasi na kuzua hofu kwa wananchi.

Amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuchukua tahadhari kubwa kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali kuhakikisha watu wanaotoka katika maeneo yenye maambukizi wanafanyiwa uchunguzi wa afya mara wanapoingia nchini.

Aidha, amesema aina mpya ya kirusi cha Ebola kilichopo sasa bado hakina chanjo maalum jambo linalohitaji wananchi kuwa waangalifu zaidi na kuepuka safari zisizo za lazima katika nchi zilizoathirika.

Amewataka wananchi kuchukua tahadhari na kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya ili kuepusha uwezekano wa kuingiza ugonjwa huo nchini.

Dk. Slim amesema Zanzibar tayari imeweka mikakati madhubuti katika viwanja vya ndege na bandarini ambapo wasafiri wote wanaingia nchini hupimwa afya zao kwa kutumia vifaa maalum vya kupima joto la mwili.

Sauti ya Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya kutoka Wizara ya Afya Zanzibar, Dk. Slim Salim Slim.

Kwa upande mwingine, Dk. Slim amesema bado kuna baadhi ya kesi za UVIKO-19 zinazojitokeza Zanzibar, huku akibainisha kuwa chanjo zimeendelea kusaidia kupunguza athari kubwa za ugonjwa huo kwa wananchi.

Sauti ya Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya kutoka Wizara ya Afya Zanzibar, Dk. Slim Salim Slim.