Zenj FM
Zenj FM
8 May 2026, 21:47

Mradi wa Zanzibar 100 Limb Project unatarajiwa kutoa miguu bandia bure kwa watu 150 waliokatwa miguu visiwani Zanzibar kuanzia Juni 1 hadi Julai 1, 2026 katika Hospitali ya Wilaya ya Mbuzini. Mradi huo unalenga kuwasaidia watu wenye ulemavu kurejea katika maisha ya kawaida na kujitegemea kiuchumi na kijamii.
Na. Mary Julius
Jamii imetakiwa kujitokeza kwa wingi katika kuhakikisha watu wenye ulemavu wa miguu wanapata fursa ya kunufaika na mradi wa Zanzibar 100 Limb Project, unaolenga kutoa miguu bandia bure kwa watu 150 waliokatwa miguu visiwani Zanzibar Kuanzia Juni 1, 2026 hadi Julai 1, 2026 katika Hospitali ya Wilaya ya Mbuzini
Akizungumza na Zenji FM, Mratibu Mkuu wa mradi huo, El Jabir Shao amesema lengo la mradi huo ni kuhakikisha watu wenye ulemavu Zanzibar wanaondokana na utegemezi na kupata nafasi ya kuendelea kutimiza ndoto zao kwa kujitegemea.
Mradi wa Zanzibar 100 Limb Project ni matokeo ya ushirikiano kati ya Naya Qadam Trust na Zanzibar Global Health & Education Foundation .
Akielezea sababu ya kuanzishwa kwa mradi huo, El Jabir amesema mhimili mkuu wa kitaalamu wa mradi ni Dr. Viquar Qurashi ambaye alianzisha taasisi ya Naya Qadam mwaka 2005 kufuatia tetemeko kubwa la ardhi nchini Pakistan.
Amesema kupitia ubunifu wa viungo bandia vinavyotumia vifaa rafiki kama PVC na raba, zaidi ya watu 10,000 duniani kote wameweza kurejea katika maisha ya kawaida na ya kujitegemea.
Aidha, Mratibu huyo amemshukuru Zarina Jafferji ambaye mchango wake mkubwa umewezesha kuletwa kwa utaalamu huo Zanzibar kupitia juhudi zake pamoja na taasisi yake ya ZGHEF.
Kwa upande wake, Mwanzilishi wa ZGHEF, Zarina Jafferji, amemshukuru mama Mariam Mwinyi kwa msaada wake mkubwa uliowezesha kufanikisha utekelezaji wa mradi huo.
Aidha ameishukuru Wizara ya Afya Zanzibar pamoja na uongozi wa Seifee Hospital Zanzibar na Hospitali ya Wilaya ya Mbuzini kwa ushirikiano wao mkubwa katika kuhakikisha maandalizi ya zoezi hilo yanafanyika kwa mafanikio.
Wananchi wote wenye mahitaji wanahimizwa kujisajili mapema ili kupata huduma hii muhimu.Namba ya usajili na maelezo: 0788 126 524.
Kauli Mbiu“Tuchukue Hatua Leo kwa Zanzibar Yenye Kujitegemea Kesho.”