Zenj FM
Zenj FM
18 May 2026, 11:31

Mkurugenzi wa ZAPONET, Asia A. Hussein amesema taasisi hiyo inatambua changamoto zinazowakabili wasaidizi wa sheria nchini ikiwemo ukosefu wa ofisi na vifaa vya kazi. Kupitia ufadhili wa Enabel Belgian Development Agency, jumuiya za wasaidizi wa sheria zitapatiwa vifaa, ofisi na mafunzo ya kuwajengea uwezo.
Na Mary Julius.
Mkurugenzi wa Mwamvuli wa Wasaidizi wa Sheria Zanzibar (ZAPONET), Asia A. Hussein, amesema taasisi hiyo inatambua changamoto mbalimbali zinazowakabili wasaidizi wa sheria nchini, ikiwemo ukosefu wa ofisi, vifaa vya kazi pamoja na mazingira yasiyoridhisha ya utoaji huduma kwa wananchi.
Akizungumza katika kikao cha robo mwaka kilichowakutanisha wakurugenzi kutoka jumuiya saba za wasaidizi wa sheria, kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi za ZAPONET eneo la Kikwajuni, amesema wengi wa wasaidizi hao wa sheria wanafanya kazi kwa kujitolea huku baadhi yao wakitoa huduma bila kuwa na ofisi rasmi.
Amesema hali hiyo imekuwa ikichangia kudharaulika kwa kazi wanayoifanya licha ya umuhimu wake mkubwa katika kusaidia wananchi kupata haki zao za msingi.
Kutokana na changamoto hizo, amesema ZAPONET imefanikiwa kupata ufadhili kutoka Enabel Belgian Development Agency ambao utasaidia jumuiya hizo kupata vifaa vya ofisini, ofisi pamoja na mafunzo ya kuwajengea uwezo ili waweze kutoa huduma bora zaidi kwa jamii.
Aidha Mkurugenzi Asia amewataka wasaidizi wa sheria Zanzibar kufanya kazi kwa bidii na kujituma, akisisitiza kuwa Serikali inathamini mchango wao katika kusaidia wananchi kupata haki na elimu ya sheria.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ZAPONET, Tatu Mvita Khamis amesema wameandaa mikakati mbalimbali ya kupunguza changamoto zinazowakabili wasaidizi wa sheria nchini.
Amesema kupitia ufadhili huo wa Enabel, wataongeza uwezo wa kuwafikia wananchi wanaohitaji msaada wa kisheria pamoja na kuboresha mazingira ya kazi kwa wasaidizi hao.
Aidha, amesema baadhi ya wasaidizi wa sheria wamekuwa wakikumbana na vitisho kutoka kwa watu wanaotaka kuwadhulumu wananchi, na kusisitiza kuwa changamoto hizo zinapaswa kuripotiwa kwa mwamvuli wa ZAPONET ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
Nao baadhi ya wakurugenzi kutoka jumuiya za wasaidizi wa sheria, akiwemo Asia Fadhili Makame na Mohammed Abdalla Mohammed wamesema kazi hiyo ya kujitolea imekuwa ikiambatana na changamoto nyingi za kiuchumi, hali inayowalazimu kutafuta njia nyingine za kujipatia kipato.
Hata hivyo, wameishukuru ZAPONET kwa juhudi zake za kuwatafutia wafadhili watakaosaidia kuimarisha jumuiya zao, huku wakiwataka wasaidizi wa sheria kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na ufanisi ili kukidhi vigezo vya wafadhili na kuendelea kuwahudumia wananchi ipasavyo.