Zenj FM
Zenj FM
11 July 2026, 23:06

Zanzibar ipo tayari kuwa mwenyeji wa Kongamano la Pili la Mafuta na Gesi Afrika (NADOGCE 2026) litakalofanyika Julai 25 hadi 27, likiwakutanisha zaidi ya washiriki 250 kutoka nchi zaidi ya 20 kujadili maendeleo ya sekta ya mafuta, gesi na nishati safi. Serikali imesema kongamano hilo litafungua fursa za uwekezaji, ajira, biashara na utalii, huku likiiweka Zanzibar kwenye ramani ya kimataifa ya sekta ya nishati.
Na Mary Julius.
Zanzibar ipo tayari kupokea Kongamano la Pili la Mafuta na Gesi Afrika (NADOGCE) linalotalajiwa kufanyika Julai 25 hadi 27, likiwakutanisha zaidi ya washiriki 250 kutoka nchi zaidi ya 20.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Blue na Uvuvi, Hamad Bakar Hamad, amesema kongamano hilo litaleta pamoja wataalamu, wawekezaji, taasisi na wadau wa sekta ya mafuta, gesi na nishati safi kujadili maendeleo ya sekta hiyo na kuitangaza Zanzibar kimataifa.
Amesema wizara itashirikiana na wadau wote kuhakikisha kongamano linafanikiwa na kufungua fursa za uwekezaji, ajira, biashara na utalii.
Naye Mwenyekiti wa Jumiya ya kimataifa ya vijana wa kiafrika katika sekta ya mafuta nna gesi YAPA, Mhandisi Jaffer Mohammed Hamza, amesema kongamano hilo litaunganisha vijana, wataalamu na wawekezaji, huku likifungua fursa mpya za ajira na uwekezaji katika sekta ya nishati Afrika.
Kwa upande wake Mratibu wa YAPA na NADOGCE 26, Mudrik Kassim Suleiman, amesema kongamano litaambatana na maonyesho ya taasisi na kampuni kutoka ndani na nje ya nchi, ametoa wito kwa wadau kuunga mkono tukio hilo.
Naye , Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa Zanzibar, Mohamed Abrahman Juma, amesema kongamano hilo ni fursa muhimu kwa vijana kujifunza na kutumia nafasi zilizopo katika sekta za madini, nishati, mafuta na gesi kwa maendeleo yao na taifa.