Zenj FM

Zanzibar yapiga hatua afya ya mama na mtoto, wajawazito 2,871 wanufaika

14 May 2026, 16:29

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar Dr. Mgereza Mzee Miraji, akizungumza katika kikao cha tathmini ya Mradi wa ZHSF Mothers/Mom Care.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto kupitia uwekezaji katika hospitali, huduma za dharura za uzazi na mifumo ya kidijitali. Kupitia Mradi wa ZHSF Mothers/Mom Care, wajawazito 2,871 wamenufaika na huduma bora za afya katika wilaya za Micheweni na Kaskazini B ndani ya mwaka mmoja.

Na Mary Julius.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar Dr. Mgereza Mzee Miraji amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, inaendelea kuweka kipaumbele maalum katika kuimarisha afya ya mama na mtoto nchini.

Akizungumza katika kikao cha wadau kwa ajili ya tathmini ya Mradi wa ZHSF Mothers/Mom Care, Katibu Mkuu amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika ujenzi wa hospitali, kuimarisha huduma za dharura za uzazi, kuongeza wataalamu wa afya pamoja na matumizi ya mifumo ya kidijitali ili kuboresha utoaji wa huduma za afya.

Ameeleza kuwa mradi huo umeleta mafanikio makubwa katika kuwafikia wajawazito, hususan katika maeneo ya vijijini na visiwani.

Ndani ya mwaka mmoja, wajawazito 2,871 wamesajiliwa katika wilaya za Micheweni na Kaskazini B na kunufaika na huduma mbalimbali za afya ya uzazi.

Katibu Mkuu amesema matumizi ya teknolojia yameongeza ufanisi katika ufuatiliaji wa afya za wajawazito na kusaidia upatikanaji wa huduma bora kwa wakati, hatua inayochangia kupunguza changamoto zinazohusiana na uzazi.

Aidha, ameipongeza PharmAccess Foundation pamoja na washirika wa maendeleo kwa mchango wao mkubwa katika kuimarisha afya ya mama na mtoto Zanzibar, huku akisisitiza umuhimu wa kuupanua mradi huo katika wilaya zote 11 za Zanzibar ili kuhakikisha hakuna mama anayebaki nyuma katika kupata huduma bora za afya ya uzazi.

Sauti ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar Dr. Mgereza Mzee Miraji.

Kwa upande wao, Mkurugenzi Mkuu wa PharmAccess Tanzania, Dkt. Heri Marwa, pamoja na Mkurugenzi wa PharmAccess Zanzibar, Dkt. Faiza Abass, wamesema kila mwaka akina mama wapatao 77 hupoteza maisha kutokana na changamoto za uzazi.

Wamesema kuanzishwa kwa Mradi wa Mfuko wa Afya ya Mama kunalenga kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na kuimarisha ustawi wa mama na mtoto.

Sauti ya Mkurugenzi Mkuu wa PharmAccess Tanzania, Dkt. Heri Marwa.
Sauti ya Dkt. Faiza Abass.
Zariha Msham Mohamed, mkazi wa Wilaya ya Kaskazini B Mkoa wa Kaskazini Unguja akizungumza katika mkutano huo.

Naye Zariha Msham Mohamed, mkazi wa Wilaya ya Kaskazini B Mkoa wa Kaskazini Unguja ambaye aliwahi kupoteza mtoto mara baada ya kujifungua kutokana na matatizo ya uzazi, ametoa wito kwa wanawake kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya na kufuata matibabu wakati wa ujauzito ili kupunguza au kuondoa kabisa vifo vya mama na mtoto.

Sauti ya Zariha Msham Mohamed,

Kauli mbiu ya mwaka huu ni:“Catalyzing Change: Advancing Maternal Health Equity in Zanzibar for a Healthier Tomorrow