Zenj FM
Zenj FM
16 April 2026, 1:22 pm

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanzisha mpango wa miaka mitano wa kujenga vituo vya kulelea watoto ili kuwasaidia kina mama wafanyabiashara katika masoko mbalimbali. Mpango huo unalenga kuhakikisha watoto wanapata malezi bora, afya njema na usalama katika mazingira rafiki.
Na Mary Julius.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imezindua Programu Jumuiishi ya Malezi na Makuzi ya Awali ya Mtoto ya miaka mitano kwa kujenga vituo vya kulelea watoto, hususan kwa watoto wa kina mama wanaojishughulisha na shughuli za kiuchumi katika masoko mbalimbali visiwani humo.
Akizungumza katika hafla ya kupokea hundi ya shilingi milioni 500 iliyotolewa na Stanbic Bank iliyo kabidhiwa kwa shirika la Save the Children, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Muhamed Mussa,amesema mpango huo unalenga kuimarisha malezi, afya na usalama wa watoto wa umri wa miaka sifuri hadi miaka nane.
Amesema utekelezaji wa mpango huo utahusisha ushirikiano kati ya wizara na taasisi zaidi ya sita zinazoshughulikia ustawi wa mtoto, huku baadhi ya maeneo yatakayonufaika yakitajwa kuwa ni pamoja na soko la Mwanakwerekwe.
Waziri Lela Muhamed Mussa ameeleza kuwa kutokana na mabadiliko ya kijamii, kimazingira na kitabia, Serikali imeona umuhimu wa kuanzisha vituo hivyo ili kuhakikisha watoto wanapata malezi bora katika mazingira salama na yenye kuzingatia maadili.
Aidha, ameipongeza Stanbic Bank Tanzania kwa mchango wake wa kifedha, kitaalamu na kimawazo katika kufanikisha mpango huo, akibainisha kuwa hatua hiyo itawawezesha kina mama kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa utulivu huku watoto wao wakipata huduma stahiki.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Fedha wa Stanbic Bank Tanzania, Derrick Lugemalila, amesema benki hiyo imetoa msaada huo kwa kipindi cha miaka mitatu ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha ustawi wa jamii na kukuza uchumi wa Zanzibar.
Amesisitiza kuwa kuwekeza kwa watoto ni msingi wa kujenga taifa imara la kesho.
Mkurugenzi wa Save the Children Angela Kauleni ameishukuru Serikali kwa kuanzisha programu hiyo ya kitaifa, ameeleza kuwa program hiyo imelenga kuboresha ustawi wa watoto pamoja na kusaidia kina mama wafanyabiashara, hususan katika maeneo ya masoko.
Kwa mujibu wa Mratibu wa Programu ya Jumuiishi ya Malezi na Makuzi ya awali ya mtoto Zanzibar Mariam Issa amesema uwepo wa program hiyo itasaidia wanawake katika kujiinua kiuchumi na kuongeza muamko wa kufanya kazi.
Amesema kutakuwepo na ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha vituo hivyo vinatoa huduma bora na salama kwa watoto.
Aidha wametoa wito kwa taasisi binafsi kushirikiana na Serikali katika kufanikisha juhudi hizo.
Wakitoa maoni yao, baadhi ya wafanyabiashara wa soko la Mwanakwerekwe wamepongeza mpango huo, wakisema utasaidia kulinda usalama wa watoto wao na kuwaepusha na changamoto mbalimbali, ikiwemo matukio ya udhalilishaji, huku ukiwawezesha kufanya kazi zao kwa utulivu na amani.
Bottom of Form