Zenj FM
Zenj FM
7 August 2026, 18:34

Mbunge wa Jimbo la Amani, Abdull Yussuf Maalim, amekabidhi vifaa vya usafi kwa vikundi vya usafi vya shehia zote nne za jimbo hilo na kuzindua visima vya maji safi katika shehia za Kwa Wazee na Kilimahewa Bondeni ili kuboresha usafi wa mazingira na upatikanaji wa maji kwa wananchi. Aidha, akiwa ameambatana na Mwakilishi wa Jimbo, Masoud Amour Masoud, walimtembelea kijana Rasam Mohamed na kumkabidhi msaada wa vifaa mbalimbali pamoja na kadi ya bima ya afya ili kumwezesha kupata huduma za matibabu.
Na Mary Julius
Mbunge wa Jimbo la Amani, Abdull Yussuf Maalim, amekabidhi vifaa vya usafi kwa vikundi vya usafi vya shehia zote nne zilizopo ndani ya jimbo hilo, sambamba na kukabidhi visima vya maji safi na salama katika shehia za Kwa Wazee na Kilimahewa Bondeni.
Hatua hiyo inalenga kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar za kuhakikisha usafi wa mazingira unaimarishwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika Amani, Abdull Yussuf Maalim amesema kuwa lengo kuu ni kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa kudumisha usafi wa miji na mazingira, hatua ambayo pia itasaidia kuifanya Zanzibar kuwa kivutio kikubwa zaidi kwa wageni na watalii.
Amesisitiza kuwa mazingira safi ni sehemu muhimu ya maandalizi ya nchi kuelekea mashindano ya AFCON yanayotarajiwa kufanyika nchini.
Katika hatua nyingine, wakati wa kukabidhi visima vya maji safi na salama katika shehia za Kwa Wazee na Kilimahewa Bondeni, Mbunge akiwa ameambatana na Mwakilishi wa Jimbo hilo, Masoud Amour Masoud, wamesema kuwa mradi huo ni sehemu ya juhudi za viongozi hao kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama ambayo imekuwa ikiwasumbua wananchi kwa muda mrefu.
Nao Baadhi ya wananchi wa Jimbo la Amani wameeleza kufurahishwa na hatua hiyo, wakisema vifaa vya usafi vitawawezesha kuendelea kutunza mazingira ya maeneo yao huku visima vya maji vikitarajiwa kuondoa adha ya ukosefu wa huduma hiyo muhimu.
Wakati huo huo, Abdull Yussuf Maalim akiwa ameambatana na Mwakilishi wa Jimbo hilo walimtembelea kijana Rasam Mohamed nyumbani kwake baada ya taarifa zake kusambaa kwenye mitandao ya kijamii zikieleza changamoto za kiafya anazokabiliana nazo.
Viongozi hao walimkabidhi msaada wa vifaa mbalimbali pamoja na kadi ya bima ya afya ili kumwezesha kupata huduma za matibabu na kuboresha ustawi wake.